Masaibu ya Rigathi Gachagua, serikali kutwaa milioni 200

Alitaja uamuzi huo kama jaribio la kuvuruga nafasi yake kama mgombea mwenza

Muhtasari

• Gachagua alisema kuwa mawakili wake watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu. 

• Alimshutumu Jaji Maina kwa upendeleo, akidai kuwa alikataa ombi lake kumhoji Mpelelezi.

• Rigathi anashukiwa kutumia washirika kupata zabuni kwa njia ya ulaghai kwa kutumia kampuni 22 akiwa ndiye mfaidi mkuu.

Mbunge wa Mathira Nderitu Gachagua
Mbunge wa Mathira Nderitu Gachagua

 Mahakama kuu siku ya Alhamisi iliagiza kutwaliwa kwa shilingi milioni 200 zinazomilikiwa na mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua. 

Mahakama ilisema kuwa mbunge huyo ambaye pia ni mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi wa Agosti, alishindwa kuthibitisha mahakamani jinsi alivyopata fedha hizo. 

Kupitia msururu wa jumbe kwenye mtandao wa Twitter Gachagua alitaja uamuzi wa Jaji Esther Maina kuwa "usio kuwa wa kushangaza mshangao" kwake na mawakili wake. 

Alimshutumu Jaji Maina kwa upendeleo, akidai kuwa "alikataa ombi letu la kumhoji Mpelelezi ili kubaini ukweli wa madai yake kwa kukiuka kanuni za ushahidi." Huku akitaja uamuzi huo kama jaribio la kutatiza nafasi yake kama mgombea mwenza wa naibu rais William Ruto.

Gachagua alisema kuwa mawakili wake watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu. 

"Uamuzi huo uliharakishwa siku kumi kabla ya uchaguzi katika jaribio lisilofaa la kudhoofisha nafasi yangu kama mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi ujao na kudidimiza umahiri wangu katika mjadala wa wagombea wenza wiki iliyopita," alisema. 

Katika uamuzi wake, mahakama ilibaini kuwa hapakuwepo ushahidi kuonyesha kuwa mbunge huyo alitekeleza kandarasi hiyo kwa yeye kupata fedha hizo. 

"Ni kweli alikiri kupokea kutoka kwa mashirika ya serikali ....hakuna chochote cha kuonyesha kuwa mkandarasi alipewa zabuni na wizara hiyo," mahakama ilibainisha.

Kulingana na Mamlaka ya Kurejesha Mali ya umma (ARA), uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Gachagua na kampuni ya Jenne Enterprises Limited walihusika katika njama ya ufujaji wa pesa za umma. Pesa hizo ziko katika Benki ya Rafiki Microfinance kwenye akaunti tatu zilizosajiliwa kwa jina la Gachagwa; moja ikiwa na shilingi milioni 165, ingine shilingi milioni 773,228 na nyingine milioni 35M. 

Rigathi anashukiwa kutumia washirika kupata zabuni kwa njia ya ulaghai kwa kutumia kampuni 22 akiwa ndiye mfaidi mkuu. 

Fedha hizo zilitoka kwa Wizara ya Ardhi, Idara ya Mipango Maalum, Wizara ya Afya, serikali ya Kaunti ya Bungoma, Hazina ya Maendeleo ya Eneo bunge la Mathira, serikali ya Kaunti ya Nyeri na Bodi ya Kitaifa ya Unyunyiziaji maji.