Mahakama ya upeo yataka kukomeshwa kwa mashambulizi dhidi ya majaji wake

Mahakama hiyo ilisema ilitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.

Muhtasari

• Mahakama hiyo ilisema kwamba, bado haijatoa uamuzi wake kamili ambao utaeleza sababu za kuidhinishwa kwa uchaguzi was Rais Mteule William Ruto.

 

Benchi la majaji saba likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, naibu CJ Lady Justice Philomena Mwilu, Jaji Mohammed Ibrahim, Jaji Dkt. Smokin Wanjala, Lady Justice Njoki Ndungu, Jaji Isaac Lenaola na Jaji William Ouko wakati wa kongamano la kesi kabla ya kuanza kwa ombi la urais katika Mahakama ya Juu Agosti 30, 2022.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Mahakama ya Upeo imetoa wito wa kukomeshwa kwa kile inachodai kuwa mashambulizi ya mara kwa mara kuhusu uamuzi wake katika kesi ya kupinga uchaguzi wa rais.

Katika taarifa ya Jumatatu, mahakama hiyo ilisema ilitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.

"Watu wanaofadhili na kutekeleza mashambulizi kwenye mitandao ya kijamii ili kuidhalilisha Mahakama wanashauriwa kuacha mara moja," ilisema taarifa hiyo.

 

Mahakama hiyo imezidi kusema kwamba, bado haijatoa uamuzi wake kamili ambao utaeleza sababu za kuidhinishwa kwa uchaguzi was Rais Mteule William Ruto.

Mahakama hiyo pia imepuuzilia mbali madai kuwa baadhi ya majaji wake wamewasilisha barua za kujiuzulu wakisema hakuna sababu ya majaji hao saba kufanya hivyo.

"Mahakama inafanya kazi kwa maelewano kama kitengo cha umoja," ilisema taarifa hiyo.

Kauli hiyo inajiri baada ya shutuma za viongozi kadhaa wa Azimio waliodai kuwa mahakama hiyo ilikuwa na mapendeleo katika uamuzi wake kuhusu kesi y akupinga uchaguzi wa urais.

Seneta wa Siaya James Orengo na mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua wametoa matamshi yaliyoashiria kwamba uamuzi wa mahakama ulikuwa wa kauli moja.

"Mtu aliyeandika hukumu hiyo amefanya udhalimu mkubwa kwa utawala wa sheria," Orengo alisema Jumapili.

Karua alisema uamuzi wa Mahakama ya Upeo ulikuwa wa mwisho lakini yeye binafsi anafikiria kwenda kwa Mahakama ya Afrika Mashariki kwa ajili ya ufafanuzi wa uamuzi wa mahakama hiyo.

"Hakuna mahali pengine ambapo tunaweza kwenda kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, lakini tunaweza kupeleka kesi mahali pengine, ili kuelewa ikiwa ni kweli mahakama yetu ilitupa haki," Karua alisema.

"Sasa sio juu ya uchaguzi, ni juu ya haki, mahakama ilisema ushahidi wetu ni puto ya hewa moto, hii inaweza kunipeleka Afrika Mashariki kujadili hukumu hiyo."

Seneta wa Busia Okiyah Omtatah pia alisema uamuzi wa mahakama kuhusu ombi la Raila unaonekana kuandikwa na jaji mmoja wa kiume wa mahakama ya upeo.

Alihusisha hili na lugha ambayo mahakama ilitumia kutupilia mbali masuala tisa yaliyoibuliwa katika malalamishi saba yaliyounganishwa.

Kulingana na mwanaharakati huyo, lugha iliyotumiwa katika hukumu hiyo ni sawa na ile inayotumiwa na jaji fulani mwanamume katika matamko yake ya kimahakama.

"Ninaomba kwamba jaji wa Mahakama ya upeo aliyeandika hukumu hiyo kubadilika. Kutupilia mbali maombi kulitosha. Unapotusi upande mmoja inamaanisha uko upande mwingine," Omtatah alisema.

Mahakama ilitumia maneno kama vile hewa moto, kukimbiza bata bukini na dhana ambayo haijathibitishwa.

Lakini mahakama ilisema uamuzi wake ulikuwa wa kauli moja.

"Mahakama ina majaji saba ambao wako huru na wanaoheshimiana kuwa ni sawa. Hukumu ya 'mmoja' ni uamuzi wa pamoja unaotolewa na mahakama na si mtu binafsi."

Mahakama iliwataka Wakenya kuwa na subira wanaposubiri hukumu kamili ambayo itatoa mwanga na ufafanuzi kuhusu misingi na mantiki ya uamuzi wake.

"Kuna kifungu cha kisheria cha siku 21 baada ya kusomwa kwa toleo fupi la hukumu kufanya hivyo," mahakama ilisema.