Jamaa auawa baada ya kukataa kufungua mlango Dagoretti

Mwili wa marehemu ulipatikana baadaye ukiwa umelala kando ya barabara ya Kinyanjui.

Muhtasari

•Boniface anaripotiwa kukataa kufungua mlango na kuuegemea na watuhumiwa wanadaiwa kugonga mlango huo kutoka nje na kumuua kutokana na kuvuja damu nyingi.

•Hakimu aliagiza kesi hiyo itajwe Oktoba 18 kwa maelekezo zaidi.

Damaris Mumbua, anayedaiwa kuwa mke, na Monica Wambui wakiwa Kibera
Damaris Mumbua, anayedaiwa kuwa mke, na Monica Wambui wakiwa Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Maafisa wa upelelezi katika eneo la Dagoretti, Nairobi wanachunguza kisa ambapo mwanamke na msimamizi wa nyumba wanashukiwa kumuua mwanamume aliyekataa kufungua mlango huko Riruta.

Mwendesha Mashtaka Ann Murage alipokuwa akiwasilisha ombi kortini la kutaka agizo la kuzuiliwa kwa Damaris Mumbua, anayedaiwa kuwa mke wa marehemu na Monica Wambui, msimamizi wa nyumba, alisema kuwa siku zaidi zinahitajika ili uchunguzi kukamilika.

"Tunaomba siku 14 kumzuilia mshtakiwa ili tukamilishe uchunguzi wetu, Bado hatujaandikisha taarifa zaidi na kufanya uchunguzi wa kimatibabu ili kujua hali ya afya ya mshtakiwa," aliambia hakimu mkazi Jacqueline Ojwang.

Mahakama ilisikia kuwa marehemu Boniface Mwenzi alikataa kufungua mlango na kuuegemea na watuhumiwa wanadaiwa kugonga mlango huo kutoka nje na kumuua kutokana na kuvuja damu nyingi.

“Marehemu alikuwa amefunga mlango wa kuingilia na kusababisha mlalamikiwa kutumia nguvu kuingia ndani ya nyumba hiyo na matokeo yake, marehemu aligongwa na kipande cha mlango wa mbao uliovunjwa nyuma ya kichwa chake na kumwacha akivuja damu nyingi na kusababisha kifo chake. ,” mahakama ilisikiza.

Mahakama ilisikia kuwa mwili wa marehemu ulipatikana baadaye ukiwa umelala kando ya barabara ya Kinyanjui.

Askari walikimbia hadi eneo la tukio na walimkuta dada ya marehemu ambaye aliwajulisha kuwa walishuku kuwa mkewe ndiye aliyehusika na tukio hilo.

Mahakamani, washukiwa hao wawili wakati wakijibu ombi hilo hawakuweka pingamizi lolote.

Waliambia mahakama kwamba walikuwa sawa na kuzuiliwa kwao.

Hakimu aliagiza kesi hiyo itajwe Oktoba 18 kwa maelekezo zaidi.