Mwanamke aliyemshutumu Linturi kwa jaribio la ubakaji aondoa kesi

Mwanamke huyo alichunguzwa na upande wa mashtaka juu ya kujitolea kwake kuondoa malalamiko.

Muhtasari

•Hakimu Mkuu Susan Shitubi alikubali ombi lake la kuondoa kesi baada ya DPP kuthibitisha kuwa wanafahamu maelezo ya makubaliano kati ya wawili hao.

•Mahakama iliagiza kwamba Sh200,000 ambazo zililipwa kama dhamana ya pesa taslimu na Linturi ziachiliwe kwake.

Aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi.
Aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi. Aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi.
Image: Jeptum Chesiyna

Mwanamke aliyemshutumu Mteule wa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kwa jaribio la ubakaji asubuhi ya leo ameondoa malalamishi yake dhidi ya seneta huyo wa zamani.

Hakimu Mkuu Susan Shitubi alikubali ombi lake la kuondoa kesi baada ya DPP kuthibitisha kuwa wanafahamu maelezo ya makubaliano kati ya wawili hao.

Shitubi aliondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha 40 cha sheria ya makosa ya kujamiiana.

Wakili wa Linturi, Muthomi Thiankolu aliambia mahakama kwamba mnamo Septemba 21 mwanamke huyo alijaza karatasi ya mahakamakuthibitisha kwamba walijadiliana na kukubali kuondoa kesi hiyo.

Wakili wa serikali Nyakira Kibera alithibitisha kortini kuwa mwanamke huyo alikubali kuondoa malalamishi na kesi dhidi ya Linturi.

Nyakira pia alithibitisha kuwa DPP alipokea hati ya kiapo iliyoapishwa na mlalamishi na hivyo kuruhusiwa kuondolewa kwa malalamishi na mwenendo wao kulingana na masharti yaliyopendekezwa na Wakili Muthomi Thiankolu.

Mwanamke huyo alikuwepo mahakamani na kuthibitisha kuwa kulikuwa na makubaliano kati yake na Linturi.

Mwanamke huyo alichunguzwa na upande wa mashtaka juu ya kujitolea kwake kwa uamuzi wao wa kuondoa malalamiko.

Alithibitisha kuwa alikubali kwa hiari kuondoa malalamiko hayo na hakukusudia kuyawasilisha au madai mengine yoyote dhidi ya washtakiwa katika siku zijazo.

Hakimu pia alimchunguza kwa kiapo na alisema alikuwa amekubali kwa hiari kuondoa malalamiko hayo bila nguvu yoyote au vitisho na kwamba hakukusudia kutoa madai mengine yoyote dhidi ya Linturi.

Mahakama iliagiza kwamba Sh200,000 ambazo zililipwa kama dhamana ya pesa taslimu na Linturi ziachiliwe kwake na pia Sh200,000 zilizochukuliwa kutoka kwake na polisi kama ushahidi.

Serikali itampatia mlalamishi na shahidi wa upande wa mashtaka simu za rununu ambazo ilichukua kutoka kwao na kuzuiliwa kwa matumizi kama ushahidi.

Mwanamke huyo alikuwa amedai kuwa Linturi aliingia katika chumba chake cha hoteli alipokuwa amelala na kujaribu kumbaka.

Septemba mwaka jana, Linturi alishtakiwa kwa jaribio la ubakaji.