Polisi 5 walioshtakiwa kwa mauaji ya mfanyibiashara Mombasa waachiliwa huru

Maafisa hao wanatarajiwa kuripoti katika afisi za IPOA mara mbili kwa mwezi.

Muhtasari
  • Aliiomba mahakama kuweka masharti yoyote ambayo  yanafaa na yameruhusiwa na mahakama
Pingu
Image: Radio Jambo

Maafisa watano wa polisi walioshtakiwa kwa mauaji yamfanyibbiashara  wa Mombasa akiwa chini ya ulinzi wa polisi wameachiliwa kila mmoja kwa bondi ya Sh1 milioni.

Maafisa hao wanatarajiwa kuripoti katika afisi za IPOA mara mbili kwa mwezi.

Watano hao wamekuwa rumande tangu Septemba mwaka jana. Ombi la awali la kuachiliwa kwa dhamana lilikuwa limekataliwa na mahakama hiyo.

Maafisa hao kupitia Mawakili wao wakiongozwa na Danstan Omari katika jaribio la pili waliiomba mahakama kuwaachilia kwa dhamana.

Aliiomba mahakama kuweka masharti yoyote ambayo  yanafaa na yameruhusiwa na mahakama.

Jaji wakati uo huo alitupilia mbali madai ya wakili huyo kwamba IPOA inatumia kesi hiyo kudhulumu haki zao. Alisema hakuna ushahidi wa athari hiyo.

Maafisa wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ni Khalif Abdulahi Sigat, James Muli Koti, Joseph Odhiambo Sirawa, Edward Kong Onchonga na Nelson Nkanae.

Marehemu-Caleb Espino-alifariki alipokuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Changamwe.

Espino alikamatwa Septemba 18, 2018, kwa kushukiwa kuwa na pombe haramu - Chang'aa na aliwekwa katika kituo hicho kama "haijulikani" mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Baadaye alifariki usiku huo baada ya polisi kudaiwa kumvamia kwa virungu vya mbao, kumpiga ngumi na mateke.

Kisha alihamishiwa katika Hospitali Kuu ya Pwani siku hiyo hiyo mwendo wa saa tisa usiku, ambapo alitangazwa kuwa amefariki alipofika.