Mahakama yatupilia mbali kesi ya ufisadi ya Ksh 7.3 Bn dhidi ya DP Gachagua

Mashtaka yalieleza kuwa kati ya 2013 na 2020, Gachagua alipokea kwa njia ya ulaghai KSh 7,330,011,265 kupitia akaunti tatu za benki.

Muhtasari

• Katika uamuzi wake Alhamisi asubuhi, Hakimu Mkuu Mwandamizi Victor Wakumile alikubaliana na upande wa mashtaka kwamba kesi hiyo haikufikia kigezo cha kusikilizwa.

Mahakama yakubali ombi la kutupiliwa mbali kesi ya ufisadi dhidi ya DP Gachagua.
Mahakama yakubali ombi la kutupiliwa mbali kesi ya ufisadi dhidi ya DP Gachagua.
Image: Facebook//RigathiGachagua

Tume ya Kupambana na Ufisadi imekubali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) la kuondoa kesi ya ufisadi ya shilingi biloni 7.3  dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hii ni baada ya DPP kuwasilisha ombi la kuondoa kesi hiyo akitaja uhaba wa ushahidi na nyaraka za kutosha kuwezesha kesi hiyo kuendelea kusikilizwa.

Katika uamuzi wake Alhamisi asubuhi, Hakimu Mkuu Mwandamizi Victor Wakumile alikubaliana na upande wa mashtaka kwamba kesi hiyo haikufikia kigezo cha kusikilizwa.

Hakimu alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulipaswa kuwa bila shaka ili kuruhusu kesi hiyo kuendelea.

"Kuna kizingiti kimoja tu cha kimantiki ambacho kinapaswa kuwa msingi wa kumfungulia mashtaka raia yeyote, hicho ni ushahidi uliotolewa uweze kuthibitisha kesi bila shaka," alisema.

Alimlaumu DPP kwa kushindwa kufanya kazi kwa kuzingatia haki na kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za kisheria.

“Kesi hizi ni shahidi wa ukweli kwamba DPP alitenda kinyume na kifungu cha 157 cha katiba kwa ujumla wake. Mtu hawezi kupendelea mashtaka kwa kutarajia ushahidi. Kupokea maombi si jambo rahisi, husababisha kunyimwa uhuru, dhihaka hadharani na inaweza kuwa msongo wa mawazo ambao unaweza kusababisha kupoteza maisha,” Wakumile alisema.

Katika ombi hilo lililowasilishwa na DPP Haji, uamuzi uliotolewa Alhamisi, Novemba 10, Hakimu Victor Wakumile aliruhusu ombi hilo lakini akaonya Gachagua na washtakiwa wenzake kwamba huenda wakakamatwa tena katika siku zijazo kwa mashtaka sawia.

“Washtakiwa wanapewa onyo hili na kuarifiwa kwamba wanaweza kukamatwa tena katika siku zijazo na kwa mashtaka yaleyale au sawa na hayo," aliamuru Wakumile.

DP Gachagua alikuwa anakabiliwa na mashtaka sita ya njama ya kutekeleza uhalifu wa kiuchumi pamoja na William Mwangi, Anne Nduta, Julianne Jahenda, Samuel Murimi, Grace Wambui, Lawrence Kimaru, Irene Wambui na David Nguru.

Kiini cha mashtaka kilikuwa katika mashtaka matano, ambapo kipindi hicho akiwa mbunge wa Mathira alishtakiwa kwa ulaghai wa kupata shilingi bilioni 7.3 kupitia akaunti yake ya kibinafsi katika Benki ya Rafiki Micro-Finance.

Mashtaka yalieleza kuwa kati ya 2013 na 2020, Gachagua alipokea kwa njia ya ulaghai KSh 7,330,011,265 kupitia akaunti tatu za benki zilizosajiliwa kwa jina la Rigathi Gachagua, zilizokuwa zikimilikiwa na Benki ya Rafiki Micro-Finance huku akijua zilikuwa sehemu ya mapato ya uhalifu.