Kesi ya mauaji ya mbunge Barasa yahamishiwa mahakama kuu ya Bungoma

Hakuna pande yoyote iliyopinga uhamishaji wa faili hiyo.

Muhtasari

•Mahakama kuu ya Kakamega imeagiza faili ya kesi hiyo kuwekwa mbele ya jaji msimamizi wa mahakama kuu ya Bungoma.

•Katika kesi hiyo, Barasa ameshtakiwa kwa mauaji ya Brian Olunga, msaidizi wa mpinzani wake Brian Khaemba.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: MAKTABA

Kesi ya mauaji ya mbunge wa Kimilili Didmus Barasa imehamishiwa katika mahakama kuu ya Bungoma.

Mahakama kuu ya Kakamega imeagiza faili ya kesi hiyo kuwekwa mbele ya jaji msimamizi wa mahakama kuu ya Bungoma.

Mahakama ilisema kwa kuwa kisa hicho kilifanyika Bungoma, ilikuwa sawa kwa kesi hiyo kufanyika huko na wala si Kakamega alikofunguliwa mashtaka.

Hakuna pande yoyote iliyopinga uhamishaji wa faili hiyo.

Afisa anayeongoza uchunguzi pia ameagizwa kuwapa mawakili wa mwathiriwa taarifa zote za mashahidi na ushahidi mwingine wa maandishi.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 24 mbele ya hakimu mfawidhi kwa maelekezo zaidi kuhusu jinsi itakavyoendelea.

Katika kesi hiyo, Barasa ameshtakiwa kwa mauaji ya Brian Olunga, msaidizi wa mpinzani wake Brian Khaemba.