Jamaa ahukumiwa kifo kwa kumuibia mlinzi, aomba kuachiliwa akahubiri neno la Mungu

Obonyo aliteta kuwa yeye ni mhubiri na alitaka kuhubiriwa neno la Mungu pindi atakaposamehewa.

Muhtasari

•Benard Obonyo alihukumiwa na hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Derrick Kuto siku ya Alhamisi baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi yake.

•Obonyo alisema hakuwahi kutenda kosa hilo, akiteta kuwa yeye ni mhubiri na alitaka kuhubiriwa neno la Mungu pindi atakaposamehewa.

:Benard Oduor Obonyo katika mahakama ya Kibera wakati wa hukumu.
WIZI KWA GHASIRI :Benard Oduor Obonyo katika mahakama ya Kibera wakati wa hukumu.
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanaume anayedaiwa kutumia nguvu kupita kiasi kumuibia mlinzi asiye na hatia baada ya kumgonga mdomoni na kumwacha akivuja damu nyingi, amehukumiwa kifo.

Benard Obonyo alihukumiwa na hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Derrick Kuto siku ya Alhamisi baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi yake.

Alikuwa ameshtakiwa kwa kutumia nguvu kumuibia Nathan Wanyonyi Sh17,000 na kadi za NHIF na NSSF, miongoni mwa vitu vingine vya kibinafsi.

Kuto alisema Obonyo hakuonyesha kujuta ingawa amekuwa na wakati wa kutosha wa kufikiria kuhusu matendo yake.

Obonyo alitambuliwa na mlalamishi na mashahidi kadhaa wakuu ambao walimweka katika kitovu cha uhalifu huo.

"Kosa hilo lilisababisha mateso ya mwathiriwa ambaye alivuja damu nyingi na, katika suala la utambulisho, mahakama inathibitisha kuwa mshtakiwa ni yule yule aliyetenda kosa hilo. Pia alikuwa manamba katika kituo cha mabasi cha Kongo huko Kawangware," Kuto alisema.

Alimhukumu kifo na kumpa siku 14 za kukata rufaa.

“Ujambazi kwa kutumia nguvu ni kosa kubwa linalovutia adhabu ya kifo na katika mazingira haya, nimezingatia kujitetea kwa mshtakiwa na hivyo namhukumu kifo. Ana siku 14 za kukata rufaa kama anavyotaka,” Kuto alisema.

Mwendesha Mashtaka Allan Mogere pia aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili kuwazuia watu wengine kutenda kosa hilo.

Katika ushahidi wake, Wanyonyi alisema kwamba alikuwa ametoka tu kazini, na alipofika Kongo katika mtaa wa Kawangware, aliandamwa na wanaume wawili waliomfuata kwa nyuma.

“Sijawahi kuzungumza nao. Mmoja wao kisha akanishika kwa nyuma na kunipiga kipigo mdomoni. Nilianza kuvuja damu nyingi,” alisema.

Wanyonyi alisema mshtakiwa alirarua kabuti lake na kuiba vitu vyake, zikiwemo pesa taslimu.

“Waliniraruria koti langu na kuniibia kadi ya NHIF, kadi ya NSSF na Sh17, 000 zilizokuwa ndani yake. Wakati huo nilikuwa na maumivu,” alisema.

Mlalamishi alisema kuwa msamaria mwema alimpeleka katika hospitali ya kibinafsi kabla ya kuhamishwa hadi hospitali nyingine.

Mashahidi wengine wakuu waliotoa ushahidi katika kesi hiyo walikuwa mtaalamu wa matibabu na afisa uchunguzi.

Katika utetezi wake, Obonyo alisema hakuwahi kutenda kosa hilo, akiteta kuwa yeye ni mhubiri na alitaka kuhubiriwa neno la Mungu pindi atakaposamehewa.

"Naomba mahakama inipe nafasi nyingine ili nihubiri neno la Mungu," alisema.