Mwanamume,50,akiri kumuoa msichana wa miaka 9

Mzee Saigilu Ololosereka, aliambia mahakama kwamba alipewa msichana huyo kwa ajili ya kuolewa na babake msichana huyo.

Muhtasari
  • Mahakama iliamua kwamba Mzee Saigilu ataendelea kuzuiliwa na polisi hadi Januari 11, 2023, hukumu hiyo itakapotolewa
Image: KNA

Mahakama ya Narok imempata na hatia mwanamume wa miaka hamsini baada ya kukiri kosa la kumuoa msichana wa miaka tisa mnamo 2019 katika eneo la Entasekera katika kaunti ndogo ya Narok Kusini.

Mzee Saigilu Ololosereka, aliambia mahakama kwamba alipewa msichana huyo kwa ajili ya kuolewa na babake msichana huyo.

Afisa wa watoto wa Narok Pilot Khaemba aliambia mahakama kuwa ndoa hiyo iligunduliwa baada ya mtoto huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 12 kupata matatizo wakati wa kujifungua na kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok kwa matibabu.

Afisa wa watoto hao aliomba korti impe afisi yake kibali cha kumhifadhi msichana huyo katika makao ya watoto ya Taraja huko Machakos pindi atakapotoka hospitalini. Ombi lao lilikubaliwa na mahakama.

Kufuatia uzito wa suala hilo, karani wa mahakama hiyo alimsomea shitaka mzee huyo kwa lugha ya Kimasai huku akimtahadharisha na adhabu hiyo kali inayoambatana na aina ya kosa alilofanya.

Jambo la kushangaza ni kwamba Mzee Ololosereka alikariri kuwa mashtaka hayo ni ya kweli na kwamba msichana huyo ni mke wake ambaye alimlinda sana.

Wakili wa serikali anayeendesha kesi hiyo aliiambia mahakama kuwa mzee huyo alikuwa mkosaji wa kwanza lakini akakariri uzito wa kosa alilotenda kwani linavutia kifungo cha maisha.

Mahakama iliamua kwamba Mzee Saigilu ataendelea kuzuiliwa na polisi hadi Januari 11, 2023, hukumu hiyo itakapotolewa.

Mahakama pia ilitoa kibali cha kukamatwa kwa wazazi wa msichana huyo ambaye alidaiwa kumuoa mtoto huyo mdogo.