Mwanamke Mkenya ashtakiwa kwa kudukua akaunti ya serikali ya Zimbabwe na kuiba bilioni 14.7

Wanadaiwa kutekeleza uhalifu huo mwezi Disemba mwaka jana.

Muhtasari

•Mwangi anadaiwa kuhamisha dola milioni 120 (Ksh 14.7 B)  kutoka kwenye akaunti hiyo hadi kwenye akaunti yake ya kibinafsi ya benki.

•Mwangi pia anakabiliwa na mashtaka mengine ya kukiuka sheria za visa kwa kufanya biashara nchini Zimbabwe ilhali yuko nchini humo kama mtalii.

Mshukiwa Primrose Nyeri Mwangi.
Image: HISANI

Mwanamke Mkenya mwenye umri wa miaka 40 anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai nchini Zimbabwe baada ya kudaiwa kuhusika katika kudukua mifumo ya shirika moja la serikali nchini humo, Zimbabwe Manpower Development Fund (Zimdef) na kuhamisha dola milioni 120 (Ksh 14.7 B)  kutoka kwenye akaunti hiyo hadi kwenye akaunti yake ya kibinafsi ya benki.

Akiwa mbele ya Mahakama ya Harare, Mwangi ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya usafiri alishtakiwa kwa kushirikiana na washukiwa wengine kudukua mifumo ya kompyuta ya Zimdef na kuhamisha kiasi kikubwa cha pesa hadi kwenye akaunti zao. Wanadaiwa kutekeleza uhalifu huo mwezi Disemba mwaka jana.

Vyombo vyaa habari vya Zimbabwe vimeripoti kuwa Mwangi na washirika wake walihamisha kiasi tofauti cha pesa kutoka akaunti ya Zimdef kwenda kwenye akaunti ya Benki ya Steward ya Maffikett Trading, akaunti ya Atrier Engineering CBZ, akaunti ya Tavaka Holding NBS na akaunti ya Newplaces Limited ya NBS.

Mtoa taarifa alifichua uhalifu huo kupitia barua pepe mnamo Desemba 28, mwaka jana na hatua ikachukuliwa. Ni dola 30,000 pekee (Ksh 3.7M) kati ya pesa zilizoibwa ambazo zimeweza kurejeshwa kufikia sasa.

Iwapo watapatikana na hatia, Mwangi na washirika wake ambao hawajulikani waliko kwa sasa wanaweza kukabiliwa na adhabu kali sana. Polisi nchini humo wanaendelea kuwasaka wenzake Mwangi. 

Mwangi pia anakabiliwa na mashtaka mengine ya kukiuka sheria za visa kwa kufanya biashara nchini Zimbabwe ilhali yuko nchini humo kama mtalii.