Chifu mstaafu afikishwa mahakamani Eldoret kwa madai ya kunajisi

Sang mwenye umri wa miaka 68 aliachiliwa kwa bondi ya shilingi laki mbili na mdhamini wa kiasi sawa.

Muhtasari

• Inadaiwa alitenda kosa hilo katika eneo la Kaptagat Kerio Valley katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet

Chifu mstaafu William Sang alipofika mbele ya mahakama ya Eldoret Januari 17 2023
Chifu mstaafu William Sang alipofika mbele ya mahakama ya Eldoret Januari 17 2023
Image: MATHEWS NDANYI

Chifu mstaafu mjini Eldoret William Sang ameshtakiwa kwa madai ya kumnajisi msichana wa shule siku ya Boxing Day mwaka jana.

Chifu huyo mstaafu alifika mbele ya hakimu mkazi mkuu Christine Menya siku ya Jumanne na kukana mashtaka mawili ya unajisi.

Inadaiwa alitenda kosa hilo katika eneo la Kaptagat Kerio Valley katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Sang ambaye pia ni afisa mstaafu wa GSU mwenye umri wa miaka 68 aliachiliwa kwa bondi ya shilingi laki mbili na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Menya aliamuru kesi hiyo itajwe Februari 6 kwa kikao cha kwanza cha kuweka mipangilio ya kusikiza kesi hiyo.

Wakati huo huo hakimu alielezea kushangazwa na ongezeko la visa vya vijana wengi kutishia kuwaua mama zao katika eneo hilo.

Aliuliza upande wa mashtaka kung’amua chanzo cha ongezeko la visa hivyo.

Alisema hayo baada ya zaidi ya vijana 10 kushtakiwa kwa makosa ya kutishia kuwaua mama zao.