Mahakama yaamuru kaburi la mwanamume kuwekwa mpakani, wake zake wakizozania mwili

Mke wa pili wa marehemu alielekea mahakamani akitaka kusitishwa kwa mazishi hadi pale atakapohusishwa.

Muhtasari

• Hakimu alisema hatimiliki ya shamba hilo itolewe ikiwa imejumuisha majina ya wanawakek hao wote waili.

Image: AFP

Mahakama moja kaitka kaunti ya Kimabu ilitoa uamuzi usio wa kawaida katika kesi ambayo iliwahusisha wake wawili wa marehemu ambao kila mmoja alikuwa anataka idhini ya kuzika mwili wa mume wao kwenye shamba lake.

Zogo lilianza pale ambapo mke wa pili alielekea mahakamani akitaka shughuli za mazishi kusitishwa mpaka pale atakapopewa idhini ya kumzika mumewe, akilalama kuwa alikuwa amefungiwa nje ya mipango na maandalizi ya mazishi.

Baada ya utata mwingi uliozingira kesi hiyo, hatimaye mahakama iliafikia uamuzi kwamba kwa vile kila mwanamke hakuwa tayari kuachia azma lake la kumzika mzee, basi kila mmoja atashiriki katika kumpa heshima za mwisho mume wao.

Kivipi?

Hakimu mkuu wa mahakama ya Thika Bi Stellah Tambu alitumia busara kama ya mfalme Suleiman na kuamuru kwamba mzee huyo atazikwa mpakani.

Kila mwanamke atatoa futi kadhaa katika mpaka wa mashamba yao marehemu aliyowagawia na kaburi kuchimbwa hapo kwenye mpaka ili kila mmoja afarijike kuwa mumewe amezikwa katika shamba lake.

“Kwamba marehemu, Christopher Mbote Chege azikwe kwenye kipande cha ardhi kinachojulikana kwa jina la LR namba 13537/101 mali hiyo hiyo. Kwa maelewano nambari mbili kwa kaburi lake litakuwa mpakani mwa ua ambalo limewekwa kama mpaka wa kutofautisha shamba la mke wa kwanza na yule wa pili, na litapimwa kwa vipimo sawa. Hiyo ina maana kuwa kaburi litakuwa katika pande zote mbili kwa usawa,” hakimu Tambu aliamuru.

Kando na hilo, mahakama pia ilitoa uamuzi wa hatimiliki ya shamba hilo atakakozikwa marehemu kutolewa ikiwa imejumuisha majina na wajane hao wawili.