Mwalimu mshukiwa aliyemuua mwanafunzi kwa kurembesha nywele kuchunguzwa akili

Ebby Noelle Samuels, mwanafunzi wa kidato cha kwanza alifariki akiwa kwenye bweni la shule hiyo, siku 2 baada ya kurejea kutoka likizoni.

Muhtasari

• Shule hiyo ilidai kuwa Ebby alifariki baada ya kuanguka kutoka kitandani, madai ambayo yalitofautiana na yale ya wanafunzi wenza walioshuhudia mwalimu akimpiga.

Mwalimu wa Gatanga CCM anayetuhumiwa kumuuwa mwanafunzi shuleni kufanyiwa uchunguzi wa kiakili
Mwalimu wa Gatanga CCM anayetuhumiwa kumuuwa mwanafunzi shuleni kufanyiwa uchunguzi wa kiakili
Image: Maktaba

Mahakama ya Kiambu imetaka aliyekuwa naibu mwalimu mkuu wa shule ya Gatanga CCM kuzuiliwa kwa siku saba zaidi ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kufnguliwa mashtaka.

Mwalimu huyo kwa jina Elizabeth Gatimu anakabiliwa na tuhuma za mauaji ya mwanafunzi kwa jina Ebby Noelle Samuels mnamo 2019 katika bweni la shule hiyo ambayo baadae ilibadilisha jina na kuitwa shule ya upili ya wasichana ya Mtakatifu Anuarite Gatanga.

Kesi hiyo imekuwa ikiendelea tangu mwaka 2019 huku uchunguzi ukifanywa na familia ya Ebby ikizidi kulilia haki kwa miaka 4 sasa.

Ebby ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha Machi 2019.

Shule hiyo ilidai kuwa mwanafunzi huyo alifariki baada ya kuanguka kutoka kitandani usiku ndani ya bweni, maoni ambayo yalitofautiana na wanafunzi wenzake ambao walitoa ushahidi wao.

Mwanafunzi huyo alifariki bwenini, wiki mbili tu baada kurejea shuleni kutoka likizo fupi kwa kile mashuhuda walisema aliadhibiwa vikali kwa kupamba na kuremba nywele zake, kinyume na kanuni za shule hiyo.

Uchunguzi wa maiti ungeonyesha baadaye kwamba Ebby alivuja damu hadi kufa baada ya kupigwa na kitu kwenye paji la uso, na kumvunja fuvu na kusababisha kuvuja damu ndani.

Mazingira hayo yalipelekea kukamatwa kwa aliyekuwa Naibu Mkuu wa shule hiyo anayedaiwa kumuua Ebby.

Mshukiwa atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri kwa siku saba akisubiri kufikishwa mahakamani, baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kiakili kubaini iwapo yuko razini kujibu mashtaka ya mauaji.