Wakili wa Fredrick Leliman kuwasilisha rufaa dhidi ya hukumu ya kifo

Ombeta alionyesha kutoridhika sana na matokeo ya kesi na hukumu ya wateja wake.

Muhtasari

• Ombeta alisema anaamini kuwa mahakama ilileta ushahidi kutoka nje ili iweze kutekeleza hukumu.

Wakili Cliff Ombeta amesema atakata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa dhidi ya wateja wake katika kesi ya mauaji ya wakili Willie Kimani.

Ombeta aliwawakilisha Fredrick Ole Leliman (mshtakiwa wa kwanza) na Stephen Cheburet Morogo (mshtakiwa wa pili) katika kesi ya mauaji ya wakili wa haki za binadamu Wille Kimani pamoja na mteja wake Josephat Mwenda na dereva wao wa teksi, Joseph Muiruri.

Akizungumza na wanahabari katika mahakama ya Milimani siku ya Ijumaa, Ombeta alionyesha kutoridhika kwake na matokeo ya kesi na hukumu ya wateja wake.

"Sisi kama upande wa utetezi, ni hukumu ambayo imekuwa ya kuhuzunisha. Ni hukumu ambayo ilitokana na ushahidi ambao haukuwapo,” alisema Ombeta.

Ombeta alisema anaamini kuwa mahakama ilileta ushahidi kutoka nje ili iweze kutekeleza hukumu hiyo.

"Tunaamini kwamba mahakama lazima ilitaka kupata mtu na hatia na hiyo ndiyo sababu ya ushahidi kuingizwa," alisema.

“Hii mahakama ilikuwa chini ya shinikizo? Je, NGOs, Chama cha Wanasheria nchini (LSK), na makundi mengine yaliiwekea shinikizo la aina fulani? Je, kweli mahakama ilitaka kuwatia hatiani watu hawa na kunawa mikono?” Ombeta aliuliza.

Ombeta alikuwa akizungumza baada ya maafisa watatu wa polisi na mdokezi kupatikana na hatia ya mauaji ya Wakili Willie Kimani.

Fredrick Leliman ambaye alikuwa mshukiwa mkuu katika kesi ya mauaji ya Willie Kimani alihukumiwa kifo.

Katika uamuzi wake, Jaji Jessie Lessit alisema kama afisa wa polisi anayelipwa kulinda maisha, alitenda kinyume na sheria.

"Mauaji hayo yalikusudiwa kuingilia haki. Walipitia mateso ya hofu na maumivu makali walipokuwa wakisubiri zamu yao ya kuuawa," alisema.