Machakos: Mwanamke afika mahakamani na kuanza kulia kama mbuzi (Videos)

Baada ya kuanza kutoa sauti kama ya mbuzi kwa mfululizo, hakimu alisitisha kesi na kuamuru asindikizwe nje.

Muhtasari

• Jane Moses, mtumizi wa Facebook ambaye alirekodi na kupakia klipu hizo mbili alielezea jinsi matukio yalianza kujiri.

 

 

 

 

 

 

 

 

Kisa kisichokuwa cha kawaida kilishuhudiwa katika mahakama ya Machakos asubuhi ya Jumatano baada ya mwanamke mshukiwa kufikishwa mahakamani na ghafla kuanza kutoa sauti kama mbuzi.

Video hiyo ilipakiwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mmoja ambaye alidai kuwa katika mahakama hiyo alisema kesi ilibidi isitishwe kwa muda kufuatia mwendelezo wa sauti za mbuzi alizokuwa akita mwanamke huyo.

Katika video hiyo, mwanamke huyo aliyekuwa amevalia sweta ya kijani alionekana akitoa sauti ya mbuzi kwa mfululizo huku makumi ya watu waliozingira eneo hilo wakibaki vinywa wazi wasijue kinachoendelea.

Jane Moses, mtumizi wa Facebook ambaye alirekodi na kupakia klipu hizo mbili alielezea jinsi matukio yalianza kujiri.

“Uchawi ni kweli. Inatokea sasa nje ya mahakama za sheria za Machakos. Huyu mama alikuwa amekuja kusikiliza kesi yake. Yeye ndiye mshitakiwa. Uvumi unasemekana anatuhumiwa kwa madai ya kumuua mtoto (bila kuthibitishwa nilikuwa katika chumba tofauti cha mahakama). Ghafla alianza kutoa sauti inayofanana na ya mbuzi mfululizo. Hakimu alilazimika kuchukua mapumziko mafupi na kuamuru asindikizwe hadi getini. Niliufuata umati uliokuwa ukimsindikiza hadi getini. Stori ya ukweli inayotokea sasa nje ya mahakama za sheria machakos,” Jane Moses aliandika.

Baadhi walisikika wakisema kwamba mwanamke huyo anafaa kupelekwa kwa maombi ili aombewe na wengine wakilonga kwamba anafaa kumtafuta mwenye mbuzi (wakikisia kuwa huenda aliiba mbuzi wa mtu).