Babu Owino anakodolea macho kifungo jela kwa kumpiga risasi DJ Evolve

Owino alikiuka sheria ya matumizi ya silaha ambayo adhabu yake ni kifungo kisichozidi mwaka mmoja jela au faini ya elfu 10 au vyote viwili.

Muhtasari

• Mwaka jana mahakama ya kesi iliruhusu uamuzi wa mwathiriwa kuondoa shtaka la kujaribu kuua.

Babu Owino na DJ Evolve
Babu Owino na DJ Evolve

Mahakama ya Milimani jijini Nairobi imempata mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na hatia ya kutumia bunduki yake vibaya na kumshambulia kwa kumfyatulia risasi mcheza santuri DJ Evolve mwaka 2020.

Hakimu Mkuu Mwandamizi Bernard Ochoi aliamua kwamba upande wa mashtaka ulitoa ushahidi wa kutoa kibali cha kumtia kwenye utetezi mbunge huyo.

Hakimu alisema mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulianzisha kesi kali dhidi ya mshtakiwa kwa kuwa alikataa madai ya mbunge huyo kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza mzigo wa ushahidi.

Mbunge huyo alishtakiwa kwa kufanya fujo akiwa amebeba bunduki kwa kufyatua risasi moja kwa nia ya kumpiga Bw Felix Orinda, almaarufu DJ Evolve katika sehemu moja ya burudani mtaani Kilimani mwaka 2020 Januari.

Upande wa mashtaka ulisema mbunge huyo alikiuka Kifungu cha 33 na 31 (1) cha Sheria ya Silaha. Adhabu ya atakayepatikana na hatia ni kifungo kisichozidi mwaka mmoja au faini isiyozidi Sh10,000 au vyote kwa pamoja.

Kuwekwa kwake kwenye utetezi sio dalili kwamba mbunge huyo ana hatia. Inamaanisha kwamba mahakama itamhitaji aeleze upande wake wa hadithi kabla ya uamuzi kutolewa kuhusu hatia yake au kutokuwa na hatia.

Mwaka jana mahakama ya kesi iliruhusu uamuzi wa mwathiriwa kuondoa shtaka la kujaribu kuua, lakini ilikubali pingamizi la upande wa mashtaka kwamba shtaka la pili la matumizi mabaya ya bunduki haliwezi kuondolewa kwa ombi la mwathiriwa.