Kinaya? Mchungaji Paul Mackenzie alia kunyimwa chakula, kupigwa na polisi katika seli

"Tumekuwa tukinyimwa chakula, ndio, na baadhi yetu hata wamekuwa wakipigwa, ndio," alilalamika.

Muhtasari

•Mackenzie na wenzake wamewashutumu maafisa wa polisi kwa kuwanyima chakula na kuwapiga wakiwa korokoroni.

•Mawakili wa washukiwa waliambia mahakama kuwa wateja wao walikuwa wakidhulumiwa korokoroni.

MCHUNGAJI PAUL MACKENZIE
Image: ALPHONSE NGARI

Mchungaji mwenye utata wa Malindi Paul Nthenge Mackenzie, mkewe Rhoda Mumbua Maweu na washukiwa wengine 16 wamewashutumu maafisa wa polisi kwa kuwanyima chakula na kuwapiga wakiwa korokoroni.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mahakama ya Shanzu siku ya Ijumaa, Mackenzie ambaye bado hajafunguliwa mashtaka rasmi alibainisha kwamba baadhi ya maafisa ambao wanawashikilia wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwaacha njaa tangu walipokamatwa kwa madai mazito dhidi yao.

"Tumekuwa tukinyimwa chakula, ndio, na baadhi yetu hata wamekuwa wakipigwa, ndio," Mackenzie alilalamika.

Washukiwa walifikishwa mahakamani siku ya Ijumaa huku upande wa mashtaka ukiomba kuwazuilia zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

Mawakili wanaowawakilisha washtakiwa, Elisha Komora na George Kariuki waliambia korti kuwa wateja wao walikuwa wakidhulumiwa korokoroni.

“Madai ya Serikali kuwa watuhumiwa waendelee kushikiliwa ili wapate lishe, ni ya upotoshaji, leo asubuhi washukiwa wote hawakupata kifungua kinywa, walinyimwa chakula kwa siku mbili tangu walipotoka mahakamani Mei 2,” alisema Komora.

Aliongeza, "Washtakiwa 3 pia walipigwa katika seli ya polisi. Kwa serikali kusema kwamba wana wakati mzuri chini ya ulinzi wa polisi ni kupotosha".

Pia alisema mkewe Mackenzie, ambaye alikamatwa na binti yao wa miaka miwili na nusu, amelazimishwa kumnunulia mtoto chakula na maji.

Paul Mackenzie, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Good News International, anakabiliwa na makosa makubwa ya mauaji, kushauri na kusaidia watu kujiua, utekaji nyara, kuendeleza itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, utapeli, ulaghai miongoni mwa mengine.

Ijumaa, timu ya mashtaka inayoshughulikia kesi dhidi yake iliomba mahakama kuruhusu serikali kumzuilia mshukiwa, na washtakiwa wenzake, kwa siku 90 zaidi ili kuruhusu kukamilika kwa uchunguzi.

Waendesha mashtaka walitoa ombi hilo mbele ya hakimu mkuu wa Shanzu Yusuf Abdallah Shikanda kwa misingi kuwa washukiwa wanaweza kuingilia upelelezi na kupata madhara baada ya kuachiliwa.

Pia waliteta kuwa hakuna hakikisho kwamba washukiwa hao watakoma kuwakaidi Wakenya wenye itikadi kali za kidini pindi watakapoachiliwa.