Mahakama yatupilia mbali kesi ya Itumbi kuomba CASs waruhusiwe kufanya kazi

Aliteuliwa kuwa CAS katika Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi wa Kidijitaji.

Muhtasari
  • Itumbi ambaye ni bloga anayeegemea mrengo tawala wa Kenya Kwanza, ni miongoni mwa walioteuliwa na Rais William Ruto.
Image: FACEBOOK// DENNIS ITUMBI

Mahakama  ya Rufaa Ijumaa imetupilia mbali  kesi ya Dennis Itumbi aliyeomba korti itoe maagizo ya kuruhusu Mawaziri Wasaidizi (CASs) 50 kuanza kazi.

Itumbi ambaye ni bloga anayeegemea mrengo tawala wa Kenya Kwanza, ni miongoni mwa walioteuliwa na Rais William Ruto.

Aliteuliwa kuwa CAS katika Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi wa Kidijitaji.

CASs waliapishwa rasmi mnamo Machi 23, 2023 lakini hawajaanza kazi kwa sababu Mahakama Kuu kwenye maagizo yaliyosomwa na Jaji Hedwig Ong’udi mnamo Ijumaa, Machi 24, 2023 iliwazima kutwaa rasmi majukumu yao hadi kesi inayopinga kuteuliwa kwao itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Aidha mahakama iliwazima kupokea mishahara, kupokea marupurupu au mafao mengine hadi kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) na Katiba Institute itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mahakama Kuu mnamo Ijumaa ilikamilisha kesi hiyo na imepanga Julai 3 kuwa tarehe ya hukumu.

"Masuala yaliyoibuliwa si muafaka kwa kupandishwa kwa rufaa katika Mahakama hii. Kushikilia vinginevyo itakuwa ni kuingia kwenye uwanja wa kesi kwa kutarajia," alisema benchi.

Kesi hiyo baadaye ilipelekwa kwa Hakimu Mkuu Martha Koome ili kuunganishwa na benchi kuamua kesi hiyo.

Kutokana na kusikitishwa na maagizo hayo, Itumbi aliwasilisha maombi katika mahakama ya rufaa.

Alisema mahakama isipositisha uamuzi wa mahakama kuu, atasalia katika hali ya 'toharani ya kikazi' kwa kuwa walioteuliwa hawawezi kuhudumu katika ofisi walikoajiriwa wala kutafuta kazi nyingine ya kuwanufaisha.