Mahakama yawaachilia waandamanaji 187 kwa dhamana

Waandamanaji hao walikamatwa Jumanne

Muhtasari

•Mahakama ya Milimani imeamuru takriban  waandamanaji 187 waliokamatwa kuachiliwa kwa dhamana.

•Jumla ya watoto 18 kuachiliwa kwa dhamana ya ksh.10,000 itakayoshikiliwa na wazazi wao na walezi wao ilhali watu wazima Ksh.50,000

Mahakama ya Milimani mjini Nairobi
Mahakama ya Milimani mjini Nairobi

Mahakama imeamuru waandamanaji waliokamatwa kuachiliwa kwa dhamana baada ya kushikwa wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2024.

Kwenye kikao cha mahakama ya Milimani Julai 3,usiku ili kusikiliza kesi ambapo watu 187 waliojumuisha watoto 18 walishtakiwa kufuatia maandamano ya Jumanne jijini Nairobi.

Hakimu mkuu mwandamizi Wandia Nyamu aliagiza kwamba watoto hao 18 waachiliwe huru mara moja kwa dhamana ya kibinafsi ya Ksh 10,000 itakayoshikiliwa na wazazi na walezi wao.

Hakimu huyo aidha, alisema kuwa haki za watoto hao zimekiukwa kwa kuwa wamewekwa kwenye seli moja na watu wazima, wengine wamejeruhiwa na hawajahudumiwa na hawajalishwa kwa muda wote waliokaa.

Hata hivyo,hakimu mkuu aliagiza kwamba watu wazima waachiliwe ifikapo saa 10 asubuhi kwa bondi za kibinafsi za Ksh 50,000 leo Julai 4. Alisema hilo linapaswa kufanywa baada ya maelezo ya kibinafsi ya walalamikiwa kuchukuliwa na maafisa wa uchunguzi.

Waandamanaji hao walifikishwa kwenye mahakama ya Milimani Julai 2 baada ya kukamatwa. Wakati wa kukamatwa kwao walikuwa wakipaza sauti  wakisema; 'Hatuna hatia'

Maandamano yamekuwa yakienea nchini kwa takriban wiki tatu sasa,huku viongozi mbalimbali kama vile naibu rais Rigathi Gachagua wakitaka vijana kukomesha maandamano.