Kabogo ataja sababu za kuungana na Ruto

Muhtasari

• Aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo alifunguka kuhusu uamuzi wake wa kuungana na Naibu Rais William Ruto chini ya Muungano wa Kenya Kwanza.

‍• Alibainisha kuwa pia aliachwa gizani kuhusu mazungumzo ambayo Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga alikuwa akifanya na rais Uhuru Kenyatta.

 

William Ruto
William Ruto

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo alifunguka kuhusu uamuzi wake wa kuungana na Naibu Rais William Ruto chini ya Muungano wa Kenya Kwanza.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Machi 22, mjini Nyeri, Kabogo alisema kuwa usiri katika muungano wa Azimio la Umoja ulimsukuma hadi kwenye kambi ya DP.

Kiongozi huyo wa chama cha Tujibebe Wakenya alisimulia jinsi ambavyo hakupewa majibu yoyote alipouliza kuhusu mipango Azimio la Umoja ilikuwa nayo kwa eneo lenye kura nyingi la Mlima Kenya iwapo wangeshinda kura ya Agosti.

Zaidi ya hayo, alibainisha kuwa pia aliachwa gizani kuhusu mazungumzo ambayo Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga alikuwa akifanya na rais Uhuru Kenyatta.

"Nimeuliza maswali na hayajajibiwa. Niliwauliza kuhusu mpango wao katika Mlima Kenya na mambo waliyojadiliana na Uhuru wakati anapostaafu na walikuwa kimya.

Hawakutaka kuzungumza juu ya mipango yao," Kabogo alisema.

Mwaniaji huyo wa ugavana wa Kiambu alieleza zaidi mazungumzo aliyokuwa nayo na DP, akieleza kuwa alishinikiza muungano huo kupitisha mtu mmoja, ugavi wa raslimali za umma kama ilivyokuwa imependekezwa katika msuada wa BBI.  

Licha ya kuambiwa kuwa haiwezekani kuidhinisha kikamilifu mtindo huo, Kabogo alisema kuwa aliahidiwa kuwa itatumika kutenga baadhi ya fedha kwa serikali za kaunti. 

"Nilimwendea Ruto na kuuliza swali lile lile na nikamwambia kuwa mtu mmoja shilingi moja ingesaidia sana eneo hili. Akajibu kuwa mtindo huo utaumiza kaunti nyingi, lakini akaniahidi kuwa pesa za ziada zitatengewa kaunti. katika utawala wake na ingegawanywa kulingana na idadi ya watu." 

Hata hivyo, Kabogo alisisitiza kwamba atahitaji kuweka kwa maandishi ya makubaliano na DP kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

 "Nataka kwa maandishi na tumekubaliana, asipoiweka kwenye maandishi, basi nitabadilisha mawazo yangu." 

Aidha alisema kuwa si hakikisho kwamba atamsaidia DP, akiongeza kuwa anaweza kubadili mawazo yake iwapo hali itabadilika. Kabogo atachuana vikali na Ferdinand Waititu (aliyekuwa gavana wa Kiambu), anayeshikilia wadhifa huo James Nyoro, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, Mbunge wa Thika Mjini Patrick Wainaina, Seneta Kimani Wamatangi na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kiambu Stephen Ndichu kuwania kiti hicho.Wanawake wawili akiwemo Dkt Juliet Kimemia na Mwende Gatabaki pia wametupa kofia zao ulingoni.