Mradi wa Maziwa Salama: Fahamu kuhusu mradi unaolenga kukupa maziwa salama

Lengo la mradi ni kuhakikisha Wakenya wanafikiwa na maziwa safi pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa wakulima.

Muhtasari

•Mradi wa Maziwa Salama (Safe Milk Project) utatumia teknolojia itakayosaidia wafugaji kubaini iwapo bidhaa zao ni salama kwa matumizi ya binadamu.

•Wakulima ambao maziwa yao yameathiriwa watapatiwa mafunzo ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa njia salama na jinsi ya kuboresha maziwa yake.

wakati wa mahojiano katika Lion Place, Westlands mnamo Juni 12, 2024.
Mtaalamu wa Usimamizi wa Miradi wa USAID Robert M. Kilonzo wakati wa mahojiano katika Lion Place, Westlands mnamo Juni 12, 2024.
Image: KEITH MUSEKE

Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) limeshirikiana na idara za serikali na kampuni za kibinafsi  kama Bio Foods na washikadau wengine katika mradi unaolenga kukuza maziwa safi katika soko la Kenya.

Mradi wa Maziwa Salama (Safe Milk Project) utatumia teknolojia itakayosaidia wafugaji kubaini iwapo bidhaa zao ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Katika mahojiano, mtaalamu wa usimamizi wa miradi wa USAID, Robert M. Kilonzo, alisema kuwa teknolojia ya kisasa haitatumika tu kubainisha usalama wa maziwa bali pia itasaidia kujua makosa ya bidhaa hizo kwa ajili ya uboreshaji na urekebishaji.

“Kuna zile teknolojia za kuangalia usawa wa maziwa ya mkulima shambani. Utaweza kutatua shida ya mkulima huyu ambaye baadaye ataweza kuleta maziwa yake pamoja ili yaweze kutayarishwa na kupakiwa,” Bw Kilonzo alimwambia mwandishi.

Alisema kuwa teknolojia ya kisasa itasaidia kubainisha iwapo mfugaji amefuata miongozo yote iliyopendekezwa ya ufugaji salama wa ng'ombe wa maziwa.

Wakulima ambao maziwa yao yameathiriwa watapatiwa mafunzo ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa njia salama na jinsi ya kuboresha maziwa yake.

“Hii teknolojia inatumika kujua kama ile masomo tumekufunza unayatimiza. Ikiwa hujatimiza, tunatumia hii maziwa kukwambia kuwa hujatimiza, uende utimize. Kwa hivyo, lengo si kukwambia hii ni mbaya utupe. Kuna masomo wapate kupokea kutoka kwa Bio Foods Pamoja na idara ya serikali katika mradi huu,” Kilonzo alisema.

Miongoni mwa miongozo ya usalama ambayo wakulima watapewa ni jinsi ya kulisha ng'ombe wao, kusafisha mikono yao, na nini cha kuepuka.

Bw Kilonzo alisema kuwa USAID inatumia taasisi binafsi kama vile Bio Foods ili kuhakikisha kuwa wakulima katika maeneo ya ndani wananufaika na Mradi wa Maziwa Salama.

Pia alisistiza kwamba lengo la mradi ni kuhakikisha Wakenya wanafikiwa na maziwa safi pamoja na kutoa mafunzo maalum yatakayowasaidia wakulima wa ngombe wa maziwa.