EXCLUSIVE!!!

Mwanadada aliyewazomea kina Mandago awajibu wanaomkosoa kwa kukataa kazi ya seneta Ledama

"Ikiwa tutarejeshewa pesa, nitachukua kazi hiyo. Lakini ikiwa sivyo, ni sawa. Nafikiri nitapoteza zote mbili na niko sawa na hilo,” Mercy alisema.

Muhtasari

•Mercy alisema anafahamu huenda akapoteza zote mbili, pesa anazotetea kurejeshewa na ofa ya kazi lakini akasisitiza yuko sawa na hilo.

•Mercy alishikilia kuwa masharti aliyompa seneta huyo wa ODM lazima yatimizwe kabla ya kufikiria kuchukua ofa yake ya kazi.

akiwasuta hadharani viongozi wa Uasin Gishu siku ya Jumatatu.
Mercy Tarus akiwasuta hadharani viongozi wa Uasin Gishu siku ya Jumatatu.
Image: HISANI

Mercy Tarus, mwanadada ambaye amepata umaarufu mkubwa baada ya video yake akiwazomea vikali viongozi wa Uasin Gishu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii amejibu baada ya kundi la Wakenya kumkosoa kwa kukataa ofa ya kazi ya seneta wa Narok, Ledama Olekina.

Katika mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu, mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Kabarak alibainisha kuwa yeye ni mtu mwenye kanuni dhabiti na hayuko tayari kubadili hilo.

Mercy alisema anafahamu huenda akapoteza zote mbili, pesa anazotetea kurejeshewa na ofa ya kazi ya seneta Olekina lakini akaweka wazi kuwa yuko tayari na yuko sawa na lolote litakalotokea.

“Mpaka tutakaporejeshewa pesa zetu. Ikiwa tutarejeshewa pesa, nitachukua kazi hiyo. Lakini ikiwa sivyo, ni sawa. Nafikiri nitapoteza zote mbili na nadhani niko sawa na hilo,” Mercy alisema.

Aliongeza, “Bila shaka, kuna watu ambao watanidhihaki . Nishaambiwa,”ingekuwa mimi, ningekuwa nishachukua kazi hiyo ingine ikae,” lakini huyo si mimi na sidhani kama nataka kuwa mtu huyo.”

Mercy alishikilia kuwa masharti aliyompa seneta huyo wa ODM lazima yatimizwe kabla ya kufikiria kuchukua ofa yake ya kazi.

Katika utetezi wake, mwanadada huyo jasiri alidokeza kuwa dhamira yake kuu kwa sasa ni kutetea kurejeshwa kwa fedha zilizotolewa na wazazi na wanafunzi kwa ajili ya mpango uliofeli wa masomo ya ng'ambo wala sio kutafuta kazi.

“Nimekataa kazi hiyo kwa heshima. Niko na masharti, masharti haya ikiwa yatatimizwa ni sawa, kama sivyo ni sawa. Sikuwa hata na lengo la hilo, nataka tu kurejeshewa pesa, "alisema.

Siku ya Alhamisi, Bi Tarus aliwashangaza wengi baada ya kukataa waziwazi ofa ya kazi aliyopewa na seneta Ledama Olekina. 

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Ledama alimsifu mhitimu huyo wa Chuo Kikuu kwa ujasiri wake na kumpa nafasi ya kumfanyia kazi.

“Mercy Tarus ningependa unifanyie kazi, speka moyo wako. Wakati ujao ni wa vijana waaminifu! Wacha tuzungumze,” Ledama alimwandikia Mercy.

Huku akimjibu seneta huyo wa Narok, Mercy hata hivyo alionekana kukataa ofa hiyo na kutoa masharti ya kutimizwa kabla ya kukubali kufanya mazungumzo na mwanasiasa huyo.

Mhitimu huyo wa chuo kikuu ambaye kwa sasa anafanya kazi ya kuuza uji na mandazi alimtaka seneta Ledama kwanza kuwaomba maseneta wenzake kuishinikiza serikali ya Uasin Gishu kurejesha pesa ambazo walikuwa wamepokea kutoka kwa wazazi kwa ajili ya mpango wa masomo wa ng’ambo uliofeli.

"Bwana. Ledama, kabla hatujaendeleza mazungumzo haya, zungumza na maseneta wenzako ili kuwajibisha Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu na kuwalazimisha KUREJESHA pesa zilizopatikana kwa bidii kwa Raia wa Kenya. Labda baadaye, tunaweza kuzungumza. Vinginevyo, sina la kusema zaidi,” Mercy alijibu siku ya Alhamisi.

Mercy alidokeza kuwa hayuko tayari kufanya kazi na seneta huyo wa ODM kwa sasa lakini akadokeza kuwa katika siku zijazo huenda akakubali ofa ya kazi kutoka kwake.

"Labda basi, tunaweza kufanya kazi kwenye mradi unaofuata kwa sababu kazi yangu itafanyika hapa. Vinginevyo, siwezi kujitolea kwa majukumu mengine," alisema.

Mercy Tarus amekuwa akivuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa siku mbili zilizopita huku wanamitandao Wakenya wakiendelea kumsifu kwa ujasiri mkubwa  ambao alionyesha wakati alipokuwa akikabiliana hadharani na gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, seneta Jackson Mandago na naibu gavana John Barorot mnamo siku ya Jumatatu.