Mwanasiasa maarufu nchini Kenya John Maina Njega amesema uongozi wa eneo la Mlima Kenya bado uko mikononi mwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Wakati akizungumza na mtangazaji Bramwel Mwololo kwenye Radio Jambo Jumatano jioni, mgombea huyo wa zamani wa kiti cha useneta wa Laikipia alibainisha kuwa rais huyo wa zamani bado hajapitisha uongozi kwa mfalme ajaye wa eneo la Mlima Kenya.
Aidha, alifichua kuwa wanapanga kuandaa mkutano ambapo Uhuru atakabidhi mamlaka kwa mrithi anayependelea wa wadhifa huo.
“Sasa hakuna kitufe kimepeanwa. Kitufe kiko na Uhuru Kenyatta. Sasa tunataka kutengeneza mkutano mmoja mkubwa sana ambapo tutamualika Uhuru Kenyatta akuje aongeleshe wananchi wa Mt Kenya,” Maina Njenga alisema Jumatano jioni.
Aliongeza, “Huo mkutano tutauweka hapo Nyeri. Uhuru Kenyatta atatoka mashimoni akuje mpaka hapo. Hapo sasa ndo atakuja na hicho kitufe apeane hapo na baada ya kupeana, kazi inaanza.”
Maina aliweka wazi kuwa wote watakuwa sawa na chaguo la mfalme ajaye wa eneo hilo ambalo rais huyo wa zamani atafanya wakati wa mkutano uliopangwa baadaye mwaka huu.
“Haitaleta fitina. Lakini sasa hivi ndio tunazungumza. Tunakubaliana kuhusu mambo yote yatakayofanyika katika mkutano huo,” Maina alisema.
Mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa hata hivyo kuna baadhi ya viongozi ambao wanapinga umoja wa eneo la Mlima Kenya na wamekuwa wakifanya juhudi kusitisha mipango yao.
Pia alidai kuwa jamii ya Mlima Kenya tayari imejuta kutokuwa na umoja wakati wa uchaguzi uliopita na kupuuza wito wa Uhuru Kenyatta wa kuwaunganisha.