- Wivu wa kupundukia katika mapenzi ni hatari
- Kuna mipaka ambayo hufai kuvuka katika uhusiano
- Mtu asiyekuamini hafa kuwa nawe katika uhusiano
- wivu wa mapenzi unafaa kuwa unaoeweka wala sio wa kutisha
Wakati unapokutana na mtu anayekuvutia ambaye unatamani kuwa naye katika mahusiano , matumaini huwa kwamba ni mtu wa kuelewa na ambaye ataheshimu mipaka na ‘uhuru’ wako hata ndani ya mahusiano yenu .
Lakini hebu jiweke katika taswira hii ambapo mpenzi wako hakuruhusu hata kwenda dukani pekee yako ,hakuruhusu kuzungumza na mwanamke yeyote na hata akiwa ni mwanamke jamaa yake basi mpenzi wako ananuna .
Ndio masaibu ya Elvis ambaye uhusiano wake na Anita umekuwa jela kwani hana uhuru wake na hata amani hana katika uhusiano wao . Wakati Anita anaposafiri kwenda kwao , sarakasi huzidi na kuwa maradufu kwa sababu wakati wote anapiga simu akimuuliza Elvis kwamba afanya nini na yuko wapi na yuko na nani . Elvis anasema wakatia mwingine imekuwa vigumu kuendelea na shughuli zake za kikazi kwa sababu ya kuvurugwa fikra kila wakati na mpenzi wake . Cha kushangaza ni kwamba anaporejea ,Anita hushtukiza tu na kuingia chumbani masaa ya kutisha kama siku moja alivyorejea nyumbani mwendo wa saa kumi alfajiri . Lengo lilikuwa kumpata Elvis akiwa na mwanamke mwingine chumbani .
Licha ya kuwa hakupata jambo lolote la kuzua shauku ,alifanya ukaguzi nyumba nzima hadi mvunguni mwa kitanda kabla ya kutulia . Elvis amesema jaribio lake la kumpa hakikisho Anita kwamba hana uhusiano mwingine wala nia ya kujihusiaha na mpenzi wa pembeni ,Anita hajatulia na wivu wake wa kimapenzi hata umevurugisha mahusiano yao na rafiki zao .
Elvis anapopokea simu hata ya mamake au mtu yeyote wa kike ,ni sharti aweke kwenye spika ili Anita ajue anazungumza na nani na asipofanya hivyo basi hawatazungumziana kwa wiki kadhaa
Anasema jaribio lake la kumtaka Anita apate usaidizi wa mshauri ili uhusiano wao uwe wa kawaida limegonga mwamba kwani pendekezop hilo kila mara linafuatwa na kununa na maandamano pamoja na mgomo baridi wa kimya chumbani huku wakikosa kuzungumziana .
Kama kuna wakati Elvis alitaka kusalimu amri kuhusu uhusiano wake na Anita bsi ni siku ambayo Anita alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia bosi wake kazini na kumtaka akome kuzungumza na Elvis kwa sababu alikuwa ameona jumbe kati yao kuhusu masuala ya kikazi lakini hilo halikutosha kumfanya ajue kwamba hamna cha ziada kati yao ila kazi .
Elvis anasema hawezi kukumbuka ni mara ngapi Anita amefungisha virago kwenda kwao na wiki oja hata haishi kabla hajarejea na hata kuapa kwamba hatorudia sarakasi zake lakini hilo huwa tu ahadi kwani hajabadilika hata kidogo .
Je ,ni kiwango kipi cha wivu wa kimapenzi ambacho mtu anaweza kustahmili?