Umaskini wasitisha uhusiano

Wazazi wake waliposikia sina chochote ,uhusiao wetu ulimalizikia papo hapo

Rono aliachiliwa hatimaye lakini mateso aliyopitia akiwa ametekwa nyara yalimfanya kuwa tayari kusalimisha amri kwa mapenzi yake kwa Fridah.

Muhtasari
  • Baada ya wazazi wa mpenzi wake kumkataa na kusema kwamba lazima angeolewa na mtu kutoka familia tajiri, wawili hao  hawakuwa na budi ila kuendelea kuonana kisiri.
  • Kwa  wiki tatu Rono alitafutwa huku kila aliyemjua akikosa kufahamu alienda wapi.

 

Hebu  fikiria iwapo  pingamizi ya penzi lako na msichana umpendaye limetoka kwa wazazi wake, kisa na maana? Kwamba huna mali .

Ndio masaibu yaliomkumba Josephat Rono mwenye umri wa miaka 28 wakati alipoanza uchumba na msichana  waliyekutana naye chuoni . Baada ya kupendana na kuanza kupanga maisha ya pamoja baadaye, ilifika wakati wa kutambulishana kwa wazazi. Kwa upande wake Rono hakuwa na tatizo kwani wazazi wake walimkubali mpezi wake Fridah na kumpa heko kwa kujishindia  mwanamke mzuri aliyeonekana kuwa mtulivu na mcha mungu. Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi kwa upande wa wazazi wa Fridah  ambao kigezo chao kikubwa kilikuwa kutaka kujua alichokuwa nacho Rono. Jaribio la  Fridah kujaribu kumtetea kwa wazazi wake  liliambulia patupu. Isitoshe, Rono alijipata matatani kwa sababu babake Fridah alikuwa afisa wa ngazi ya juu wa polisi ambaye alifahamika kote na kumkaidi ingekuwa ni jambo hatari .

Baada ya wazazi wa mpenzi wake kumkataa na kusema kwamba lazima angeolewa na mtu kutoka familia tajiri, wawili hao  hawakuwa na budi ila kuendelea kuonana kisiri. Kitu ambacho hawakugundua ni kwamba babake Fridah kwa sababu ya cheo chake, alikuwa amewatuma makachero wake kumfuatilia na kuchunguza hatua zake zote na kisha kumpripoti. Walipokutana kila mara,  Fridah angeambiwa na babake kwamba anafaa kukoma kuendelea kumuona Rono. Msichana katika mapenzi hashauriki na hivi  waliendelea kuonana na Rono. Hamaki ya mzee ilipanda siku moja na  bila kujua alichokuwa akipanga, babake Fridah alifanya mpango wa Rono kutekwa nyara .

Kwa  wiki tatu Rono alitafutwa huku kila aliyemjua akikosa kufahamu alienda wapi. Wazazi wake Rono walipofahamu chanzo cha msaibu ya mtoto wao, walienda kumrai babake Fridah amuachilie Rono huku wakiapa kukatiza uhusiano kati ya mtoto wao na Fridah.

Rono aliachiliwa hatimaye lakini mateso aliyopitia akiwa ametekwa nyara yalimfanya kuwa tayari kusalimisha amri kwa mapenzi yake kwa Fridah. Makovu ya kuzuiwa kufunga pingu za maisha na  msichana aliyempenda yamemfanya Rono hadi sasa kuhofia kujiingiza katika uhusiano mwingine tangia hapo .