MFAHAMU TB JOSHUA

Mambo sita ambayo hukuyajua kumhusu Mhubiri TB Joshua

Shirika moja la kutetea haki liliwasilisha malalamiko baada ya kukagua video zisizopungua saba zikimuonesha mhubiri huyo akifanya maombi ya "kuwaponya" watu wa mapenzi ya jinsia moja

Muhtasari

•Alikuwa miongoni mwa wahubiri wakubwa nchini Nigeria ambaye hakukubaliwa na wenzake licha ya kuwa na wafuasi wengi barani Afrika.

•Baadhi ya watu wamekuwa wakimkosoa kutokana na idadi ya miujiza yake aliyofanya katika mikutano yake.

TB Joshua
TB Joshua
Image: Hisani

Mhubiri maarufu wa Nigeria TB Joshua alipata umaarufu mkubwa katika kazi yake ya uinjilisti na kujipa wafuasi kote Afrika.

Hata hivyo kuna mengi ambayo watu hawakuyajua kumhusu TB Joshua ambaye kifo chake jumamosi iliyopita kiliwaacha wengi wakiwa na mshangao 

1. Hakupendwa na wenzake

Imeelezwa kuwa TB Joshua aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 57 alikuwa miongoni mwa wahubiri wakubwa nchini Nigeria ambaye hakukubaliwa na wenzake licha ya kuwa na wafuasi wengi barani Afrika.

Kanisa la TB Joshua
Kanisa la TB Joshua
Image: Facebook

Alitengwa na Chama cha Wakristo wa Nigeria (CAN) na Wapentekoste wa Nigeria (PFN) huku sababu mbalimbali zikitajwa licha ya kuwa hakuwa tofauti na wahubiri wengine waliokuwa wakihubiri katika televisheni na kuwateka raia wa Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 90.

"Joshua ambaye alikuwa kiongozi wa kanisa la Synagogue Church Of All Nations (SCOAN) hakuwa mmoja wao. Alikuwa mkali. Hakuogopa lolote. Njia zake hazikuwa za kawaida," amesema Abimbola Adelakun, profesa msaidizi katika idara ya mafunzo katika Chuo Kikuu chaTexas.

Joshua alianza mahubiri kwenye televisheni miaka ya 90 na wafuasi wake walimuona kama mtu wa kuaminiwa na mnyenyekevu na ujumbe wake ulienea duniani kote.

"Hawaamini kwamba unaweza kujisimamia mwenyewe bila kuwa na mtu wa kumtegemea," amesema Gbenga Osinaike, mchapishaji wa taasisi kuu ya uchapishaji wa vitabu ya Kanisa la Kipentekoste nchini Nigeria.

TB Joshua aliyezaliwa Juni 12, 1963 anatajwa kama mhubiri ambaye hakutumia nguvu katika shughuli zake za kiroho lakini maombi yake yalionekana kuwa na nguvu.

2. Mke wake Evelyn Joshua pia ni mhubiri

Nabii Evelyn Joshua
Nabii Evelyn Joshua
Image: FACEBOOK

Nabii Evelyn Joshua aliyekuwa mke wa Temitope Balogun Joshua , alituma ujumbe wake kwenye ukurasa wa Twitter akimuomboleza mume wake ulioonekana kuwatia moyo waombolezaji wengine , kufuatia kifo cha mumewe.

Nabii Evelyn Joshua ni mke wa TB Joshua, Mhubiri wa televisheni tajiri na mwanzilishi wa kanisa la Synagogue, Church of All Nations.

Alizaliwa tarehe 17 Disemba 1968 katika eneo la Okala Okpumo, Jimbo la Delta nchini , Nigeria, kwa wazazi wake Bwana na Bibi Nicholas Akobundo.

Kwa hivyo basi mwezi Juni, 2021 Evelyn Joshua anatimiza umri wa miaka 52.

Evelyn Joshua alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya St Emecheta iliyopo katika mji wa Ezi, katika jimbo la Delta nchini Nigeria.

Mwaka 1977, alihamia katika mji wa Lagos na kuendelea na masomo yake katika shule ya msingi ya Orile na baadaye akaendelea na masomo ya sekondari.

Alipohitimu, alipata fursa ya kufanya kazi katika kampuni ya Nigerian Distilleries Ota, iliyopo katika jimbo la Ogun.

3. Umaarufu wa watoto wake

Ndoa ya Mchungaji TB Joshua na Evelyn Joshua ilizaa matunda, kwani waliweza kubarikiwa na watoto watatu, wawili miongoni mwao wakiwa maarufu.

Kulingana na Bi Evelyne TB Joshua, mume wake, hakujali sana suala la jinsia ya watoto wake licha ya kwamba watoto wa kiume huangaliwa kwa namna ya kipekee katika utamaduni wa jamii yake.

Serah Joshua Serah, mwanae mkubwa kati ya mabinti zake watatu, ni muhitimu wa mafunzo ya sheria katika Chuo Kikuu cha masuala ya kiuchumi London School of Economics na kwa sasa anasomea Shahada yake ya uzamifu (PhD).

Alisajiliwa katika baraza la mawakili nchini Nigeria kama mwanasheria anayefanya kazi hiyo mwezi Disemba 2015.

Serah aliolewa na mwanaume wa Kitanzania mjini Arusha mwaka 2021.

Mwanae Promise pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha London School of Economics akisomea masomo ya mahusiano ya kimataifa na siasa . Promise kwa sasa anasomea Shahada ya uzamili.

Mtoto wa mwisho mdogo kati ya watoto wa Evelyne hafahamiki, kwani hakuna taarifa zinazomuhusu.

4. Alijihusisha sana na uhisani

TB Joshua
TB Joshua
Image: Twitter

Jumamosi ijayo ya tarehe 12 Juni mhubiri wa Nigeria Temitope Balogun almaarufu TB Joshua angeadhimisha miaka 58 ya kuzaliwa kwake .

Lakini kwa bahati mbaya aliaga dunia siku ya Jumamosi tarehe 5 Juni wiki moja tu kabla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa .

Alitangaza kwamba mwaka huu hakuwa na nia ya kusherehekea siku hiyo kwasababu hakufurahia yote yaliyokuwa yakitendeka duniani .

Alisema: " Haitakuwa rahisi kwangu kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa,kwasababu watu wengi wanahangaika duniani'

" Huzuni zao na hofu zao zipo nami hivyo basi siku hiyo itakuwa ya sala na kufunga na tusiwasahau wanaohitaji msaada wetu'.

Aliongeza kwamba 'kulikuwa na siku zake nyingi za kusherehekea kuzaliwa kwake. Kando na kuonekana kujali mahangaiko ya watu wasiojiweza duniani pia alikuwa na miradi mbali mbali ya uhisani iliyoendeshwa na kanisa lake

5.'Miujiza' yake ilivyozua utata

TB Joshua
TB Joshua
Image: Facebook

Baadhi ya watu wamekuwa wakimkosoa kutokana na idadi ya miujiza yake aliyofanya katika mikutano yake.

Baraza la makanisa ya Pentecostal nchini Nigeria PFN , chini ya mwavuli wa makanisa ya Pentecostal nchini Nigeria halikubaliani na kanisa la mhubiri huyo wakimtaja TB Joshua kuwa kibaraka.

Christ Okote mhubiri wa kanisa maarufu nchini Nigeria alimshutumu Joshua kwa kuwa 'mganga'

Wakosoaji wake wa Kikristo wanasema kwamba mbinu zinazotumiwa na Joshua haziendani na zile za biblia.

Lakini mzozo uliokuwa ukimzunguka muhubiri huyo haukuishia hapo, kwasababu wengi pia walimkosoa kuhusu miujiza yake mingi katika mikutano yake.

Mwaka 2017, Chris Okotie, muhubiri Maarufu nchini Nigeria , alimshutumu Joshua kwa kufanya 'uganga'.

Lakini waziri wa zamani wa usafari wa ndege , Femi Fan Kayode ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa TB Joshua alimtaka Okotie kuwacha kumshambulia Joshua na badala yake kuitisha umoja katika kanisa hilo.

Wakosoaji wake wa Kikristo wamekuwa wakisema kwamba mbinu anazotumia TB Joshua haziendani na zile zilizopo katika bíblia.

Baraza la Kanisa la Pentecostal nchini Nigeria halikukubali kanisa la Joshua kuwa chini yake.

6. Msimamo wake kuhusu wapenzi wa jinsia moja

YouTube ilisimamisha akaunti ya TB Joshua juu ya madai ya matamshi ya chuki.

Shirika moja la kutetea haki liliwasilisha malalamiko baada ya kukagua video zisizopungua saba zikimuonesha mhubiri huyo akifanya maombi ya "kuwaponya" watu wa mapenzi ya jinsia moja

Facebook pia iliwahi kuondoa moja ya machapisho ambayo yanaonesha mwanamke akipigwa kofi wakati TB Joshua akimuombea na kusema anatoa "roho ya pepo".

Akaunti yake ya YouTube ilikuwa na wafuasi milioni 1.8.

Shirika la Open Democracy lenye makao yake nchini Uingereza liliwasilisha malalamiko baada ya kukagua video saba zilizochapishwa kwenye idhaa ya YouTube ya TB Joshua Ministries kati ya 2016 na 2020, ambayo inaonysha kuwa mhubiri huyo anafanya maombi "kuponya" watu wa mapenzi ya jinsia moja.

Msemaji wa YouTube aliambia OpenDemocracy kwamba akaunti hiyo ilifungwa kwa sababu sera yake "inakataza maudhui ambayo yanadai kwamba mtu ni mgonjwa wa kiakili, anaugua, au ni duni kwa sababu ya ushirika wao katika kikundi kinacholindwa pamoja na mwelekeo wa kijinsia".

Ujumbe kwenye akaunti ya Facebook ya TB Joshua Ministries uilisema: "Tumekuwa na uhusiano mrefu na wenye mafanikio na YouTube na tunaamini uamuzi huu umefanywa kwa haraka."

(Uhariri na Samuel Maina)