Fahamu utajiri wa bilionea marehemu Naushad Merali

Mwaka wa 2015, Forbes ilimtangaza kama nambari tatu kwenye orodha ya Wakenya tajiri zaidi akiwa na utajiri wa bilioni 39.96 kwa wakati huo

Muhtasari

•Sameer Group iko na kampuni tanzu zaidi ya kumi na tano zikiwemo Sasini Tea & Coffee, Sameer Africa Ltd, Sameer Business Park, Sameer Industrial Park, Swift Global Kenya Ltd, Eveready East Afica Ltd, Equatorial Investment Bank, Savanna Coffee Lounge, Ryce East Africa, Sameer Agriculture & Livestock(Kampala, Uganda) kati ya kampuni zingine.

Naushad Merali
Naushad Merali
Image: Hisani

Siku ya Jumamosi, Wakenya waliomboleza kifo cha mmoja wa wanabiashara ambao wameweza kubobea nchini na kote ulimwenguni.

Dkt Naushad Noorali Merali aiaga asubuhi ya Jumamosi akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi kulingana na ujumbe uliotolewa na familia yake.

Marehemu alizaliwa mwaka wa 1951 nchini Kenya na kulelewa na kusomea  humo.

Bila shaka, Merali alikuwa miongoni mwa watu tajiri zaidi nchini na kote duniani.

Mwaka wa 2015, Forbes ilimtangaza kama nambari tatu kwenye orodha ya Wakenya tajiri zaidi akiwa na utajiri wa bilioni 39.96 kwa wakati huo. 

Forbes ilimuorodhesha kama nambari 48 kwa utajiri barani Afrika kwa wakati huo.

Utajiri wake ulitoka wapi?

1. Kencell (Bharti Airtel Kenya)

Merali alikuwa mwanzilishi wa kampuni ya huduma ya simu ya Kencell mwaka wa 2000 akishirikiana na kampuni ya  Vivendi ya Ufaransa.

Mwaka wa 2004 alinunua asilimia 60% ya umiliki wa kampuni hiyo kutoka kwa Vivendi kisha kuuzia Celtel na kutengeneza faida ya $20M.

Kencell ilikuja kubadilishwa jina baadae na kuitwa Celtel, na kwa sasa inajulikana kama Airtel.

Hata hivyo, Merali aliuza hisa zake katika kampuni hiyo mwaka wa 2014 na kujiuzulu kama mwenyekiti.

2. Sameer Group

Merali alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya Sameer Group ambayo inahusiana na ukulima, ujenzi, usafirishaji , fedha na teknolojia.

Makao makuu ya kampuni hiyo yako Nairobi ingawa huduma zake zinaenda mpaka nje ya mipaka ya Kenya.

Sameer Group iko na kampuni tanzu zaidi ya kumi na tano zikiwemo Sasini Tea & Coffee, Sameer Africa Ltd, Sameer Business Park, Sameer Industrial Park, Swift Global Kenya Ltd, Eveready East Afica Ltd, Equatorial Investment Bank, Savanna Coffee Lounge, Ryce East Africa, Sameer Agriculture & Livestock(Kampala, Uganda) kati ya kampuni zingine.

3. WPH Kenya Tea Company

Merali alikuwa mkurugenzi katika kampuni ya WPH Kenya Tea Company kutoka mwaka wa 1980.

4. Hisa

Merali aliaminika kuwa na hisa katika kampuni mbalimbali nchini Kenya .

Hisani

Merali pamoja na bibi yake Zarin Merali walikuwa na shirika la kuwasaidia Wakenya wasiojiweza kwa jina Zarin and Naushad Merali Foundation.

Kupitia Merali $ Zarin foundation, wawili hao walisaidia mayatima na watoto ambao hawakuwa na uwezo wa kupata masomo. Walipatiana misaada kwenye sekta ya elimu na matibabu.