Fahamu tofauti kati ya Eid ul-Fitr na Eid ul-Adha

Eid Mubarak kwa Kiarabu maana yake ni "sherehe au sikukuu njema au yenye Baraka".

Muhtasari

•Eid ul-Fitr maana yake ni "sikukuu ya kumaliza mfungo" na kutumiwa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

•Eid al-Adha maana yake ni "sikukuu ya kutoa kafara/kuchinja" kwa Kiarabu na hutumiwa kukumbuka wakati nabii Ibrahimu alipotaka kumtoa kafara mwanawe Ishmael alivyoamriwa na Allah, lakini akapewa kondoo na Mungu amtoe kafara badala yake.

•Eid Mubarak kwa Kiarabu maana yake ni "sherehe au sikukuu njema au yenye Baraka".

Image: GETTY IMAGES

Karibu watu milioni 2.5 huelekea miji mitakatifu ya Makka na Madina kila mwaka kwa ibada ya kuhiji. Lakini kwa sababu ya virusi vya corona, Saudi Arabia imepiga marufuku mahujaji kutoka nchi za nje kuingia nchini humo na kuruhusu idadi ndogo tu ya wenyeji kushiriki kwenye ibada hiyo.

Kutamatika kwa ibada ya Hijja huadhimishwa kwa sherehe maalumu za Eid.

Hijja huwa inahitaji mtu kuwa mzima wa kimwili na uwezo wa kifedha wa kuweza kufanya ibada hiyo angalau mara moja katika maisha ya muumini.

Huu ni mwaka wa pili mfululizo nchi ya Saudi Arabia inapiga marufuku raia wa kugeni kwenda kuhiji.

Lakini je tofauti iliyopo kati ya Eid ul-Fitr na Eid ul-Adha ni ipi?

Eid ul-Fitr

Eid ul-Fitr maana yake ni "sikukuu ya kumaliza mfungo" na kutumiwa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Sikukuu hii ya Eid-ul-Adha ya mwaka 2019 kuna waliosheherekea tarehe 11 na wengine tarehe 12 Agosti.
Sikukuu hii ya Eid-ul-Adha ya mwaka 2019 kuna waliosheherekea tarehe 11 na wengine tarehe 12 Agosti.
Image: GETTY IMAGES

Siku hii huwa ni siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mengi yenye waumini wengi wa Kiislamu. Hata hivyo idadi ya siku za mapumziko huwa tofauti katika nchi mbalimbali.

Waislamu huanza sherehe hizi kwa kukusanyika kwa maombi ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya macheo.

Ni kawaida kuwaona Waislamu wakikusanyika katika misikiti na viwanja vya wazi kwa maoni ya pamoja.

Kabla ya ibada hiyo, huwa wanatoa sadaka kwa maskini (huitwa Zakat) ambayo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya Kiislamu.

Ni kawaida kwa miji mikuu mataifa ya Kiislamu kupambwa sana na sherehe kubwa kuandaliwa, watoto kununuliwa nguo mpya na kupewa zawadi mbalimbali.

Siku hii huadhimishwa baada ya kuonekana kwa mwezi wa Shawwal.

Waislamu wakiwa uwanja wa Nyakabiga, Bujumbura wakati wa kusherehekea Eid ul-Fitr 2018
Waislamu wakiwa uwanja wa Nyakabiga, Bujumbura wakati wa kusherehekea Eid ul-Fitr 2018
Image: HISANI

 

Eid ul-Adha

Eid al-Adha ndiyo sikukuu kuu zaidi ya kidini miongoni mwa Waislamu kote duniani na pia huwa ni siku ya mapumziko mataifa mengi yenye Waislamu.

Nchini Kenya Eid ul-Fitr huwa ni siku ya mapumziko lakini Eid ul-Adha awali haikuwa siku ya mapumziko lakini katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiadhimishwa kama siku ya kitaifa na watu hupumzika.

Kondoo , waliopangwa tayari kwa kutolewa kafara, wakitazamwa na muislam mjini Beijing, Uchina mwaka 2017
Kondoo , waliopangwa tayari kwa kutolewa kafara, wakitazamwa na muislam mjini Beijing, Uchina mwaka 2017
Image: GETTY IMAGES

Eid al-Adha maana yake ni "sikukuu ya kutoa kafara/kuchinja" kwa Kiarabu na hutumiwa kukumbuka wakati nabii Ibrahimu alipotaka kumtoa kafara mwanawe Ishmael alivyoamriwa na Allah, lakini akapewa kondoo na Mungu amtoe kafara badala yake.

Sikukuu ya Eid ul-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhul Hijjah.

Ibada ya Hajj kwenda Mecca huanza siku mbili kabla ya Eid al-Adha na tarehe yake huthibitishwa baada ya kuoenakana kwa mwezi huo wa Dhu al-Hijjah.

Eid al-Adha ina majina mbalimbali katika mataifa ya Kiislamu:

 

Mamilioni ya waislamu huhudhuria Ibada ya Hijjah huko Mecca kila mwaka
Mamilioni ya waislamu huhudhuria Ibada ya Hijjah huko Mecca kila mwaka
Image: GETTY IMAGES
  • Eid el-Kabir nchini Nigeria na Morocco
  • Tabaski nchini Senegal na Gambia.
  • Kurban Bayrami nchini Uturuki
  • Hari Raya Haji nchini Indonesia, Malaysia na Singapore.
  • Eid è Qurbon, nchini Iran.
  • Bakr-Id or Qurbani Eid, nchini India, Bangladesh, na kwa Kiurdu pia.
  • Idi kubwa nchini Tanzania

Waislamu pia huvalia mavazi yao mazuri na ya kupendeza siku hii na huenda msikitini kwa maombi.

Baadhi humchinja ng'ombe, mbuzi au kondoo kukumbuka kitendo cha imani cha nabii Ibrahimu.

Hula chakula chenye nyama na huwapa jamaa, majirani na maskini nyama ya mnyama waliyemchinja.

Katika baadhi ya mataifa na miji hairuhusiwi watu kuwachinja wanyama kwao nyumbani hivyo vichinjio hutumiwa. Waislamu pia hutoa pesa za hisani kipindi hicho.

Waislamu hutumia Eid ul-Adha kusherehekea utiifu kamili wa nabii Ibrahimu kwa amri ya Mungu na kuwakumbusha wenyewe kuwa tayari kutoa kafara chochote ili kutimiza maagizo ya Mungu na kumfuata.

Eid Mubarak

Chakula au mlo wa pamoja ndio kitu kinachozingatiwa zaidi wenye sikukuu hii
Chakula au mlo wa pamoja ndio kitu kinachozingatiwa zaidi wenye sikukuu hii
Image: GETTY IMAGES

Chakula au mlo wa pamoja ndio kitu kinachozingatiwa zaidi wenye sikukuu hii

Eid Mubarak kwa Kiarabu maana yake ni "sherehe au sikukuu njema au yenye Baraka".

Ni salamu za kawaida wakati wa sikukuu za Eid.

Wakati wa Eid ul-Fitr, salamu nyingine maarufu ni

  • Ciid wanaagsan - Somalia.
  • Mutlu Bayramlar - Uturuki.
  • Selamat Idul Fitri - Indonesia.
  • Selamat Hari Raya - Malaysia, Brunei, na Singapore.
  • Barka da Sallah - baadhi ya maeneo ya Nigeria.