Mambo yaliyofichuka kumhusu afisa Caroline Kangogo kwenye hafla ya mazishi yake

Wanafamilia na marafiki waliohudhuria hafla hiyo walimtaja Bi Caroline kama mtu aliyekuwa mpole na mwema.

Muhtasari

•Rekodi za shule ya msingi aliyosomea Caroline zinaashiria kuwa alikuwa mwanafunzi mwenye nidhamu na alihudumu kama kinara.

•Kakake marehemu, Mark Kangogo alisema kuwa dadake  alikuwa mtu mzuri licha ya yale yaliandikwa kumhusu kwenye vyombo vya habari.

•Chifu wa eneo hilo alisema kuwa mengi yalikuwa yamesemwa kumhusu Caroline ila walikuwa wameachia Mungu yote.

Afisa Caroline Kangogo azikwa nyumbani kwa wazazi wake Elgeyo Marakwet
Afisa Caroline Kangogo azikwa nyumbani kwa wazazi wake Elgeyo Marakwet
Image: MATHEWS NDAYI

Hatimaye afisa Caroline Kangogo aliyedaiwa kujitoa uhai kwa kujipiga risasi mnamo Julai 16 alizikwa nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Nyawa kaunti ya Elgeyo Marakwet siku ya Alhamisi.

Afisa huyo ambaye alihusishwa na mauaji ya wanaume wawili alizikwa katika hafla tulivu iliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji ikiwemo maafisa wa polisi zaidi ya 20 kutoka kituo cha polisi cha Nakuru alikokuwa anahudumu marehemu.

Hata hivyo, saluti 21 za bunduki hazikuwepo kama ilivyo desturi katika mazishi ya polisi yeyote  aliyeaga nchini.

Marehemu alizikwa akiwa amevalishwa gauni la harusi kama alivyokuwa ameomba kupitia ujumbe wa simu ambao aliacha kama ameandika.

Mambo mengi kumhusu marehemu yalifichuka kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye miharara ya bonde la Kerio.

Wanafamilia na marafiki waliohudhuria hafla hiyo walimtaja Bi Caroline kama mtu aliyekuwa mpole na mwema.

Pale kijijini alifahamika kama 'Chemu' ambacho ni kifupisho cha jina lake Chemutai.

Marehemu alisomea katika shule ya msingi ya Nyawa ambayo iko mita chache tu kutoka nyumbani kwa wazazi wake.

Rekodi za shule hiyo zinaashiria kuwa marehemu alikuwa mwanafunzi mwenye nidhamu na alihudumu kama kinara.

"Labda alipatwa na matatizo mengine alipojiunga na huduma ya polisi ila rekodi zetu zinaashiria kuwa alikuwa mwanafunzi mzuri sana" Mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa sasa alisema.

Wanafamilia wengi hawakuamini kuwa 'Chemu' waliyejua ndiye alitekeleza mauaji ya wanaume wawili mapema mwezi huu.

Wazazi wa Caroline Bw Barnaba Kangogo na Bi Leah Kangogo walishindwa kuhutubia waombolezaji labda kwa kulemewa na majonzi ya kupoteza mtoto wao.

Msemaji wa familia, Robert Kipkorir alihutubia waombolezaji kwa niaba ya familia.

Alisema kuwa walikuwa wamesikitishwa na kuathirika sana na mambo yaliyozingira kifo cha mmoja wao.

"Kama familia hatujui kilichofanyika kwani hatukuamini kuwa bado ni Caroline tuliyemjua. Alitajwa kama mkimbizi hatari na ilituuma sana. Polisi watatuambia ukweli," Kipkorir alisema.

Alisema kuwa ni maombi yake jambo kama hilo lisimfanyikie mtu mwingine.

Kakake marehemu, Mark Kangogo alisema kuwa dadake  alikuwa mtu mzuri licha ya yale yaliandikwa kumhusu kwenye vyombo vya habari.

"Kama alitekeleza mauji yale kama ilivyoripotiwa basi ni vibaya. Hata niliuliza maafisa wakuu waliokuwa wanahudumu naye na walisema kuwa Caroline alikuwa afisa mzuri" Mark alisema.

Chifu wa eneo hilo alisema kuwa mengi yalikuwa yamesemwa kumhusu Caroline ila walikuwa wameachia Mungu yote.

Naibu gavana wa Elgeyo Marakwet Wesley Rotich aliomba serikali kuangazia njia za kusuluhisha misongo ya mawazo miongoni mwa maafisa wa usalama.

Baadhi ya wanafamilia  walidai kuwa  hawakuwa wameridhishwa na  upelelezi uliokuwa unaendelea  na pia matokeo ya upasuaji wa mwili uliofanywa na mwapatholojia wa serikali Johansen Oduor.

Oduor alifanya upasuaji wa mwili wa Caroline  mapema wiki hii ni kudai kuwa risasi ilimwingia marehemu kwenye upande wa kulia wa kichwa na kutokea upande wa kushoto.

Hata hivyo alidai kuwa uchunguzi zaidi ungefanywa kubaini kama kwamba alijipiga risasi mwenyewe ama alipigwa na mtu mwingine.