Yavunja moyo! Wanasiasa, wasanii mashuhuri waongoza maandamano mitandaoni dhidi ya mauaji ya ndugu wawili Embu

Maelfu ya wanamitandao walijawa na ghadhabu wamelaani idara ya polisi na kudai mabadiliko kufuatia kile wanachosema kuwa mauji ya kiholelaholela.

Muhtasari

•Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia walizikwa jana (Agosti 13) nyumbani kwao katika kijiji cha Kithangari kaunti ya Embu.

•Raila Odinga, Moses Kuria na Justin Muturi ni baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamedai haki ya ndugu hao wawili kupatikana huku Akothee, Otile Brown, King Kaka, Njugush, Brenda Wairimu, Massawe Japani, Betty Kyalo , Teacher Wanjiku na Bahati wakiwa miongoni mwa wasanii ambao wametoa hisia zao na kufariji familia ya marehemu.

Image: HISANI

Maandamano dhidi ya kifo cha ndugu wawili kutoka Embu waliaoga katika hali tatanishi yameendelea kunoga mitandaoni.

Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia walizikwa jana (Agosti 13) nyumbani kwao katika kijiji cha Kithangari kaunti ya Embu.

Maelfu ya Wakenya ikiwemo viongozi wa kisiasa na wasanii mashuhuri wameendelea kulaani mauaji ya ndugu hao wawili na kudai haki ipatikane kwa familia yao.

Picha zinazoonyesha mama ya vijana hao wawili, Catherine Wawira akiwezwa na hisia za majonzi na kuangua kilio kikubwa mbele ya waombolezaji wakati wa mazishi imevunja nyoyo za Wakenya wengi ambao wameshinikiza idara ya upelelezi kufanya hara kupata majibu kuhusiana na tukio hilo.

Maelfu ya wanamitandao walijawa na ghadhabu wamelaani idara ya polisi na kudai mabadiliko kufuatia kile wanachosema kuwa mauji ya kiholelaholela.

Raila Odinga, Moses Kuria na Justin Muturi ni baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamedai haki ya ndugu hao wawili kupatikana huku Akothee, Otile Brown, King Kaka, Njugush, Brenda Wairimu, Massawe Japani, Betty Kyalo , Teacher Wanjiku na Bahati wakiwa miongoni mwa wasanii ambao wametoa hisia zao na kufariji familia ya marehemu.

Kinara wa ODM Raila Odinga alifariji familia na kusema  kuwa hakuna mzazi anafaa kupitia yale familia ya Ndwiga imepitia

"Kwa familia ya Ndwiga ambayo imezika watoto wao Emmanuel na Benson leo, pokeeni rambirambi zangu. Maombi yangu yanamuendea mama ya marehemu, Catherine Wawira,. Nasimama pamoja na kilio chenu kama mzazi. Hakuna mzazi anafaa kupitia yale ambayo mmepitia. Kama kitengo cha haki dhidi ya jinai kitawahi kufanya kazi basi kifanye kwa ajili ya familia. Naungana na mwito huo" Raila aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amemwagiza rais Kenyatta kutupilia mbali amri ya kutotoka nje kama njia  ya kuonyesha mshikamano katika juhudi za kutafuta haki ya Njiru na Mutura.

"Rais Uhuru Kenyatta. Ili kuonyesha mshikamanano na #KianjokomaBrothers, tunakuagiza kuondoa kafyu mara moja. Walikuwa wanajaribu tu kutafuta faida kubwa kutoka kwa biashara yao ya kuuza nyama. Waliuliwa na wakatili wako wanaovaa nguo za bluu wakiwa kazini yao. Kazi yao ya kuuza nyama ya nguruwe ni muhimu pia. Maliza kafyu sasa!" Kuria alisema

Mtangazaji Massawe Japani alisema kuwa machozi ya mama ya vijana hao hayakumwagika bure na Mungu angemlipishia kisasi.

"Mungu halali.. machozi yake sio ya bure. Naomba Mungu amlipishie." Massawe aliandika.

Betty Kyalo amesema kuwa mauaji ya ndugu hao ni ya kinyama na ya kuhuzunisha  na kutoa shinikizo haki itendeke.

"Mauaji haya ni ya kusikitisha, ya kinyama na ya kuvunja moyo. Tunafaa kukasirika. Haki lazima itendeke. Hawa vijana walikuwa wadogo na hawakufaa kupatana na yaliyowakumba mikononi mwa maafisa wa usalama" Betty aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Hizi hapa jumbe za baadhi ya wasaniii wengine:-

Mungu alaze nyoyo za Njiru na Mutura pema peponi.