Fahamu jinsi Wakenya wanavyotumika kufanya udanganyifu Ulaya

Muhtasari

•Ripoti hii kutoka Nairobi inaangazia kuhusu waandishi wanaowasaidia wanafunzi wa kigeni kudanganya katika masomo yao.

Image: BBC

Mwanafunzi wa London au New York akienda mtandaoni kumlipa mtu amfanyie uandishi wa kitaaluma, kuna uwezekano mkubwa wa kazi hiyo kufanywa na mtu kutoka nchini Kenya.

Ripoti ya BBC Trending kutoka Nairobi inaangazia kuhusu waandishi wanaowasaidia wanafunzi wa kigeni kudanganya katika masomo yao.

Kennedy alikuwa mwalimu lakini katika kipindi cha miaka mitano amejikwamua kimaisha kupitia njia tofauti. "Nafanya uandishi wa kitaaluma," anasema.

Yeye ni sehemu ya tasnia ya kimataifa mtandaoni, ambayo ni biashara kubwa nchini Kenya.

Lakini kile anachofanya Kennedy na Wakenya wengine wengi wanaita "uandishi wa kitaaluma", kwengine duniani kinaitwa udanganyifu.

Ikiwa wewe ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu au mwanafunzi wa shule ya upili ambaye anasumbuka kufanya zoezi la masomo, basi Kennedy na timu yake ya waandishi watakufanyia- kwa ada stahiki.

Wakimaliza watakupa uwasilishe zoezi hilo kana kwamba umefanya mwenyewe bora usijulikane.

Wale wanaondesha biashara hiyo wanafahamika kama "essay mill" Tovuti, ambazo zinatumiwa na wanafunzi wanaofanya udanganyifu kutuma kazi zao wanazotaka kufanyiwa.

Baadhi ya tovuti hizo ziko Marekani na Ulaya Mashariki na wale wanazoziendesha wanaweza kujipatia faida ya hadi nusu ya ada inayotozwa wateja.

Kiwango anachotozwa mteja kinategemea zoezi analotaka kufanyiwa. Zoezi likiwa rahisi ada ni kidogo lakini likiwa gumu kama vile kufanyiwa nadharia nzima ya PHD bila shaka ada anayotozwa mteja ni ya juu.

 

Baadhi ya wanafunzi wanatumia mitandao inayotoa huduma hiyo kufany audanganyifu
PA MEDIA Baadhi ya wanafunzi wanatumia mitandao inayotoa huduma hiyo kufany audanganyifu

Kennedy na waandishi wake alio waajiri wanakamilisha hadi insha 200 au mitihani ya mtandaoni kwa mwezi.

"Unajiunga na mtandao kwa kutumia nambari ya usajili ya mwanafunzi na kumfanyia mtihani" anaongezea.

Watafiti ambao husoma biashara ya kile kinachoitwa "udanganyifu wa mkataba" wanasema Kenya ni kitovu muhimu.

Sababu ni rahisi: Kenya ni nchi inayozungumza na mfumo mzuri wa elimu ambapo mara nyingi kuna fursa duni za kiuchumi, haswa kwa vijana.

Njia pekee ya vijana kujikimu kimaisha ni kutumia elimu yao kuwasaidia raia wa kigeni kufikia malengo yao.

Picha za wasifu wa waandishi wa kukodisha kwenye tovuti zinazotoa huduma ya uandishi wa kitaaluma zinaashiria kuwa waandishi wote ni wazungu.

Lakini ukweli ni kwamba ukiomba kufanyiwa uandishi wa kitaaluma mtandaoni kuna uwezekano wa kazi hiyo kufanywa na Mkenya.

Kwa Kennedy, kujiunga na tasnia hiyo ilikuwa wazo zuri. Kennedy aliye na umri wa miaka 30 anajipatia karibu shilingi elfu 150 za Kenya (karib £1000) kwa mwezi- kiwango kikubwa kidogo kuliko mashahara wa wastani - na karibu mara nne ya mshahara aliyokuwa akipokea alipokuwa mwalimu.

Lakini anajihisi vipi kwamba anasaidia kudhoofisha uadilifu wa elimu kote duniani?

Kama mwalimu wa zamani anajihisi "kuathiriwa kimaadili" lakini anasema kwamba anafanya kwa ajili ya kujipatia kipato. "Ninajali, lakini najali nini zaidi ya maisha yangu mwenyewe - wakati mwingine lazima uishi kwanza kufikiria maadili, "anasema.

Kennedy anajua vizuri kuwa kazi yake inaweza kumsaidia mteja kudanganya hadi wakapata shahada ambayo itawapatia ajira itakayowalipa."Halafu unatambua sio mashindano dhidi yao. Wakati mwingine ni mashindano dhidi ya umaskini."

 

David anajifadhili mwenyewe kusoma kwa kuwafanyiwa wanafunzi wa kigeni kazi zao za masomo
BBC David anajifadhili mwenyewe kusoma kwa kuwafanyiwa wanafunzi wa kigeni kazi zao za masomo

Ijapokuwa kuna waandishi wa kitaaluma wa kukodishwa katika nchi zingine, wale wa Kenya wamebuni mbinu yao binafsi ya kuendesha kufanya kazi hizo.

Kuna makundi ya "waandishi wa kitaaluma" katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Telegram ambapo kazi na programu tumishi zinauzwa. Baadhi ya makundi hayo yana maelfu ya wanachama. Zinajumuisha wataalamu wa kiwango cha wastani ambao wanafanya kazi huku wakiendelea na masomo.

David ni mmoja wa watu 10 walio katika mwaka wao wa mwisho katika Chuo Kikuu ambaye anajifadhili mweyewe kupitia njia hiyo.

"Wazazi wangu hawana uwezo wa kugharamia maisha yangu chuoni,"anasema. "Kwa hivyo nimejiunga na tasnia hii kama njia ya kujikimu kimasomo na hata kusaidia familia yangu ."

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, David amekuwa akiwaandikia wanafunzi wa Uingereza na Marekani ambao ni wateja wake karibu insha 360.

Anaandika kurasa 15 kwa siku kwa ada ya shilingi 250 kw(£1.65) kwa kila ukurasa. "Naweza kufany akazi kutoka Jumatatu hadi Ijumaa usiku na mchana, lakini natenga wikendi kuangazia masomo yangu"

Kazi hiyo imemwezesha kukunua kipande cha ardhi kijijini kwao na kuwaajiri watu wa kumfanyia shughuli ya kilimo -ambayo anasema ni uwekezaji wa siku za usoni.

David amepewa kandarasi na mtu mwandamizi zaidi katika tasnia hiyo ambaye ana akaunti ya uandishi kwenye moja ya tovuti kubwa ya waandishi wa kitaaluma wa kigeni.

Lakini kupata akaunti si rahisi. Kampuni zingine zinasisitiza juu ya waombaji kuwa uthibitisho wa kupita mitihani ya masomo.

Tangazo la kibishara katika akaunti ya uandishi wa kitaaluma ambayo inauzwa katika kundi la Facebook la black Kenyan writer
Tangazo la kibishara katika akaunti ya uandishi wa kitaaluma ambayo inauzwa katika kundi la Facebook la black Kenyan writer
Image: FACEBOOK

Akaunti zilizo na hakiki nyingi za wateja kwa nyota tano ni bidhaa muhimu na hununuliwa na kuuzwa katika vikundi vya uandishi wa kitaaluma.

Hivyo ndivyo wanafunzi huhadaiwa. Huenda wakafikiria wanafanyiwa uandishi wao wa kitaaluma na mwandishi ambaye anaujuzi mkubwa.

Lakini kwa kweli huenda ni mtu ambaye alinunua akaunti kutokana na sifa nzuri

"Nimenunua zaidi ya akaunti 10," anasema Kennedy. "Baadhi ya akaunti hizo zinagharimu shilingi 500,000 za Kenya sawa na (£3,300). Hakuna njia nyingine ya kupata wateja."

Kuwa na akauntu ni kitu ambacho David anatazamia baada ya kuhutimu masomo yake. Akiwa na miaka 23 tu tayari ameanza kukuza kizazi kijacho.

Anawapa mafunzo waandishi wa kimasomo na kuwapitishia kazi rahisi waanze kupata uzoefu. "Kutokana na hilo tulijenga usuhuba na kusaidiana. Kwa hivyo ni tasnia ambayo inakua."

Wengine hawavutiwi na taaluma hiyo. John alijiingiza katika uandishi wa masomo baada ya kuhitimu. Anatarajia kuachana nayo baada ya kupata kazi ya uandishi katika vyombo vya Habari.

"Kuna watu hufanyiwa kazi ya uuguzi. Singelipenda kwenda hospitali kutibiwa na mtu ambaye alimlipa mtu mwingine kumfanyia mitihani. Unajua ni hatari sana. Kwa kweli inanitia hofu sana,"anasema. "Iinastahili kufutiliwa mbali."

Dkt Gladys Nyachieo, mhadhiri wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Multimedia jijini Nairobi, anaamini jukumu la kukabiliana na udanganyifu chuoni liko kwa nchi Tajiri ambazo wanafunzi wao ndio wateja wakuu. Bila mahitaji kama hayo hakungekuwa na usambazaji.

Dkt Gladys Nyachieo anasema mataifa Tajiri yanastahili kuchukua hatua dhidi ya uovu huo
Dkt Gladys Nyachieo anasema mataifa Tajiri yanastahili kuchukua hatua dhidi ya uovu huo
Image: MULTIMEDIA UNIVERSITY

"Ikiwa wangeweza kuchukua hatua kwa mfano kupiga marufuku husuma ya uandishi wa kitaaluma upande mmoja,basi udanganyifu unaweza kupunguzwa,"anasema.

Baadhi ya nchi zinachukua hatua. Mwaka jana, Australia ilipiga marufuku huduma ya kuuza insha.

Sheria kama hiyo pia inazingatiwa nchini Uingereza. Lakini bado haijabainika jinsi sheria hiyo itakavyotumika kukomesha biashara ambayo inavuka mipaka ya kimataifa kwa urahisi.

Kwa sasa Dkt Nyachieo anajaribu kushughukia suala hili kadri ya uwezo wake.

"Nawaambia wanafunzi wangu hayo sio maadili. Sio sawa," anasema. "Lakini tunaweza kufanya hilo tu. Ndio njia ya kuishi kwa watu wengine. Kwa hivyo ni tatizo kubwa."

Baadhi ya majina katika taarifa hii yamebadilishwa