Haki ya utoaji mimba: Maelfu waandamana kutaka utoaji mimba uhalalishwe kisheria

Muhtasari
  • Maelfu ya watu wameandamana katika majimbo yote 50 ya Marekani kuunga mkono haki ya utoaji mimba
Image: BBC

Maelfu ya watu wameandamana katika majimbo yote 50 ya Marekani kuunga mkono haki ya utoaji mimba.

Wameamua kuandamana kupinga sheria mpya iliyopitishwa katika jimbo la Texas ambayo inatoa masharti kwenye ya kutoa mimba kwenye jimbo hilo.

Wanaounga mkono haki ya utoaji mimba nchini humo wanahofu kwamba kuweka masharti kwenye utoaji wa mimba ni kurudisha nyuma haki za kikatiba. Wanataka mtu awe huru kutoa mimba ya umri wowote ambao mtoto hawezi kuishi, bila kuwekewa masharti yoyote ya sheria.

Katika miezi inayokuja Mahakama kuu inatarajia kuanza kusikiliza kesi ambayo inaweza kubatilisha uamuzi wa 'Roe v Wade' wa mwaka 1973 ambao ulihalalisha utoaji mimba nchini kote.

Huko Washington DC, waandamanaji walikusanyika kwenye majengo ya Mahakama wakiwa na mabango yaliyoandikwa"Halalisheni utoaji mimba".

Hata hivyo wakati maandamano hayo yalipoanza, yalikabiliwa na mamia ya watu wengine ambao wanapinga utoaji mimba kuhalalishwa.

"Damu za watoto wasio na hatia ziko mikononi mwenu!" alisema kwa sauti mtu mmoja, lakini alimezwa na nyimbo na makelele ya wanaounga mkono, gazeti la Washington Post limeripoti.

Mwanamke mmoja aliyekuwa kwenye maandamano hayo ya kuunga mkono haki ya mwanamke kuwa na uchaguzi kwenye masuala yanayohusu mwili wake alisema; "Bahati mbaya sijawahi kuwa kwenye chaguo la kutoa mimba, kuna wanawake wengi, ambao serikali wala wanaume hawapaswi kuwasemea linapokuja suala la miili yetu," Robin Horn aliiambia Reuters.

Maandamano hayo yameandaliwa na walioandaa maandamano mengine makubwa ya Women's March - ya kwanza yaliyokusanya mamilioni ya watu walioandamana siku moja baada ya kuapishwa kwa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mwaka 2017.

"Aina hii ya matukio husadia kuwafikia watu wengi nchini," alisema Rachel O'Leary Carmona, Mtendaji mkuu wa Women's March.

"Wengi wetu tumekuwa tukifahamu kwamba utoaji mimba litakuwa jambo halali kisheria na ruksa kwa kila anayetaka," aliongeza.

Katika jimbo la New York state, Gavana Kathy Hochul alijitokeza kwenye maandamano na kusema. "Nimechoshwa kupigania haki za utoaji mimba," alisema mwanamama huyo na kuongeza: "Ni sheria iliyowekwa nchini na hamuwezi kutupokonya haki hiyo , sio sasa wala milele".

Maandamano mengine yalifanyika huko Austin, Texas, ambapo Septemba mosi mwaka huu ilipitishwa sheria inayokataza utoaji mimba unaofikia umri ambao mapigo ya moyo ya mtoto yameanza.

Sheria hiyo inayoitwa 'Heartbeat Act' pia inampa mtu haki ya kumshitaki daktari ambaye atamtoa mtu mimba ambayo imevuka wiki sita (mwezi mmoja na wiki mbili. Wanaoiunga mkono sheria hiyo, wanasema inalenga kumlinda mtoto.

Watetezi wengi wa haki za binadamu wanaitaka mahakama kuu kuizua sheria iliyopitishwa Texas.

Disemba 1 mwaka huu, Mahakama inatarajia kusikiliza kesi iliyofunguliwa kupinga sheria ya Mississipi inayopinga utoaji mimba iliyofikia umri wa wiki 15, kama miezi minne kasoro.

Hukumu katika kesi hiyo huenda ikapindua uamuzi wa mahakama wa mwaka 1973 'Roe v Wade' ambayo ilitaka kulindwa kwa haki ya utoaji mimba. Ambapo hukumu hiyo iliruhusu kutoa mimba ya umri wowote mpaka kufikia angalau wiki 28 ama umri ambao mtoto hata akitoka anaweza kuishi. Nyuma ya hapo unaruhusiwa kutoa mimba ambayo umri wake mtoto hawezi kuishi, akiwa nje ya mfuko wa uzazi.