Simulizi:- 'Maumbile yangu ni ya kiume lakini jinsia yangu ni ya kike'

Muhtasari

•Kwa kuwa mama yake alimpokea kama binti licha ya kuwa na nyeti ya kiume pia , familia yake ilimlea kama binti mpaka anapoingia shuleni.

Image: BBC

Maisha yake Sharon Ngeru ni kama hadithi ya kufikirika. Huwezi kusema ni jambo la hali halisi - Ni kana kwamba ni simulizi isiyo ya kweli lakini ukweli wa mambo ni kuwa Sharon alizaliwa kama huntha (mwenye jinsia mbili -ya kike na ya kiume) ! Wakati anazaliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita alipewa jina la Sharon Wamuhu Ngeru , hili ni jina la Kike .

Kwa kuwa mama yake alimpokea kama binti licha ya kuwa na nyeti ya kiume pia , familia yake ilimlea kama binti mpaka anapoingia shuleni.

"Nilizaliwa kama huntha(mtu mwenye jinsia mbili) , nikalelewa kama mtoto wa kike , ila kwa wakati huu mimi ninaishi nikijitambua kama mwanamume ambaye nina nyeti za kike. "Sharon anasema .

Hadi wakati Sharon anapobaleghe hakuwa na habari kwamba alikuwa mtoto tofauti na wenzake , alipofikisha umri wa miaka 13 mabadiliko ya mwili wake yalianza kuashiria kwa kiasi kikubwa kwamba jinsia iliokuwa na ushawishi mkuu mwilini mwake ni ya kiume na sio ya kike aliyolelewa nayo.

Kwa mfano anasema kwamba sauti yake ilianza kubadilika na kuwa nzito kama mwanamume anayekomaa , viungo vyake kwa mfano misuli ilianza kubadilika kama ya kiume. Ila wakati haya yanafanyika tayari mchakato wa upasuaji ulikuwa umeanza tangu akiwa mtoto mdogo.

Sharon anasema kuwa , kwasababu alikuwa na nyeti za kiume na kike , wazazi wake waliamua aondolewe ya kiume na asalie na ya kike pekee.

"Wakati nimeanza kubaleghe nilikuwa na mahangaiko mengi mno , kwani mwili wangu ulianza kubadilika ukiegemea upande wa kiume zaidi , ila kiashiria cha jinsia yangu kilikuwa kimesalia cha kike baada ya upasuaji. Sasa tatizo ni kuwa nilianza kumeza tembe za homoni kila siku kamą njia ya kuhakikisha kuwa niliegemea upande huo , upande ulioamuliwa na wazazi wangu kwani nilikuwa mchanga , upasuaji ambao ulikuwa unipe unafuu wa maisha uligeuka na kuwa mkanganyiko mkuu wa maisha yangu "anasema Sharon

Maisha ya Sharon yalichukua mkondo mwengine baada ya ugunduzi kuwa yeye anajihisi kama mwanamume ila anaishi kama mwanamke tangu akiwa na miaka 13 hadi leo siku baada ya siku anaishi kama mfungwa ndani ya mwili wake.

Changamoto ya maumbile yake

Image: BBC

Kila mara Sharon anapowazia kunapambauka kwa siku nyingine yeye huwazia hadi mitaa atakayopitia na ni akina nani atakuwa akitangamana nao.

Hii ni kutokana na changamoto yake kuu imetokana na mtazamo wa baadhi ya watu katika jamii anayoishi kuhusu yeye.

Sharon anasema kuwa hali ya maumbile ya kuwa huntha inakuwa na mahangaiko mengi , kutokana na watu kumuona huntha kama kiume cha ajabu. Wakati uamuzi kuhusu upasuaji wake ulipofanywa alikuwa mtoto na anadai kuwa hakupewa habari za kutosha kuhusu hali yake .

"Sehemu walioiondoa ndio ilikuwa inifae katika utu uzima , sasa mimi ninaishi na hisia za mwanamume lakini nina sehemu za siri za mwanamke hii inanitesa sana. Sasa maisha kama haya mtu anaelekea wapi jamani?" anahoji Sharon .

Sharon kama huntha anasema wakati ameanza kugundua tatizo la maumbile yake alikuwa anauliza maswali mengi lakini hakuna aliyekuwa anampa majibu yaliyo sahihi. Ni bibi yake kwa upande wa mama ambaye alikaa naye chini na kuzungumza naye kabla hajaaga na kumweleza kuwa alizaliwa na hali hiyo .

"Bibi yangu alipata ujasiri na kunieleza ukweli wa mambo kunihusu , haikuwa rahisi kwake lakini alinisaidia kuanza kujikubali, alinieleza kuwa sina budi ila kujibali nilivyo , kwa kuwa tayari marekebisho ya upasuaji yalihitilafiana na uhalisia wangu", Sharon anasema.

Baada ya Bibi yake kufariki Sharon alijikakamua kuendelea na maisha yake , licha ya kuwa wengi katika jamii yake hawamuelewi.

Image: BBC

Changamoto nyingine na ambayo ni hatari zaidi ni ile ya kuparamiwa na kushambuliwa na umma.

Katika kisa kimoja ambacho anakumbuka ni kuwa siku moja akiwa mtaani alibanwa na haja ndogo akiwa jijini Nairobi , kwa kuwa anautambulisho wa jinsia ya kike yeye aliingia kwenye vyoo vya wanawake , ghafla baadhi ya wanawake aliokutana nao mle ndani walianza kupiga mayowee wakisema kuwa alikuwa mwanamume aliyekuwa na nia ya kuwabaka .

Ni kısa kilichosababisha watu kumtoa nje ya vyoo na kuanza kumvua nguo , ili kudhibitisha jinsia yake. Sharon anaeleza kuwa hata baada ya umati huo kushuhudia yeye anajinsia ya kike walimuacha papo hapo bila nguo.

Ni moja ya visa vingi ambavyo amekumbana navyo , kisa kingine anasema ni wakati alipotembelea hospitali moja kwa ajili ya huduma za vipimo. Wahudumu waliitana mmoja baada ya mwingine kujionea maumbile yake. Sharon anasema kuwa licha ya kuwa alihitaji kufanyiwa vipimo anahisi kuwa wahudumu wale pia walitumia fursa hiyo kumkejeli mumbile yake .

"Kuna siku nyingine, nilikuwa na shughuli zangu mitaani, ghafla mwanaume mmoja alinishambulia na kunivua nguo, alikuwa anapiga kelele akisema kuwa maumbile yangu hayaeleweki , baada ya kushuhudia alichopania pia yeye aliondoka tu na aibu ya kuvuliwa nguo. Ndio maisha ya huntha wengi hasa vijijini na mijini ambapo hawana uhuru licha ya kuwa serikali ya Kenya inatutambua kama jinsia ya tatu huru "Sharon anasema.

Hisia za kimapenzi

Changamoto kubwa ambayo Sharon anapitia ni kuwa anahisia za kimapenzi za kiume kumaanisha kuwa yeye hupenda wanawake. Anasema hilo linakuwa ni tatizo kwa kuwa licha ya kuwa na hisia za kiume na homoni za kiume lakini ana viungo vya kike .

"Mimi ni mwanaume niliyebeba nyeti za kike kwa sababu ya upasuaji , nina mpenzi wangu ninayempenda sana na huwa hatuna uhuru wa kutangamana kwa umma kamą wapenzi kutokana na mtazamo ambao utaibuka, ni maisha magumu Sana Sana,"Sharon anasema.

Image: BBC

Kwa nyakati hizi Sharon huvalia mavazi ya kiume , kwani yeye amechagua kuishi kama mwanamume . Changamoto inayojitokeza ni utambulisho wake , hasa wakati anahangaika kutafuta ajira , anasema kuwa amenyimwa ajira mara nyingi kwa kuwa anaambiwa haeleweki yeye ni nani.

"Wakati mmoja niliajiriwa kama mfanyakazi wa nyumbani , nilijitambulisha kamą mwanamke , ila nilieleza mwajiri wangu hali yangu , ila kwa kumueleza aliishia kunidhalalisha na kunitusi kuhusu hali hiyo , alikuwa ananitusi na kuharibu hadhi na utu wangu kila siku , alinieleza kawa afadhali mnyama mmoja kuliko binadamu wa aina yangu " Anakumbuka Sharon. Kwa miaka miwili alivumilia kufanya ile kazi kwa kuwa hakuwa na chaguo..

Kenya imewasajili watu wa jinsia moja kirasmi na walihesabiwa kama huntha na wala sio kwa jinsia ya kike au ya kiume . Inakadiriwa kuwa kuna karibu watu zaidi ya 700,000 wa jinsia mbili wanaoishi nchini Kenya.

Kwa takwimu hizi za mwaka jana, Kenya itakuwa taifa la kwanza barani Afrika kuwatambua watu hawa ambao wanajiona watu wa kawaida.

Je hali kuwa na jinsia mbili inasababishwa na nini ?

Image: BBC

Maelezo ya wataalam ni mengi kuhusiana na hali hii ; kulingana na mtandao w verywellhealth.com ambao una maelezo ya kina kuhusu hali ya huntha kuwa ni; maumbile ya watu wanaozaliwa na nyeti mbili au huntha ni neno la jumla linalotumiwa kuelezea mtu yeyote aliye na maumbile ya kijinsia au ya kibaolojia ambayo ni tofauti zaidi kuliko maumbile ya jadi yanayohusu miili ya kiume au ya kike.

Kuzaliwa na hali hiyo uhusisha Jinsia ambazo zinaonekana kuwa za ajabu, haya yakichangiwa aidha na kromosomu, mifumo ya homoni, sehemu za siri, au mfumo wa uzazi wa ndani.

Tofauti hizi, ambazo wakati mwingine hujulikana kama utofauti katika ukuaji wa kijinsia au shida za ukuaji wa kijinsia , zinaweza kuonekana wakati wa kuzaliwa au zinaweza kutambuliwa hadi baadaye maishani, kama wakati wa kubaleghe au wakati wa kujaribu kuwa na mtoto.

Wakati mwingine mtu hajui kamwe kuwa ana tofauti hizi hadi baadaye maishani .

Matibabu ya hali hii ni pamoja na upasuaji wa sehemu ya siri kwa ujumla. Lakini Upasuaji huu haupaswi kufanywa wakati wa utoto isipokuwa kuna suala la dharura la matibabu.

Inapaswa hadi pale mtu anapobaleghe na ishara za kuafikia utu uzima huashiria uhalisia wamaumbile yake kwa undani, hapo anaweza kufanyiwa upasuaji.