Zifahamu helikopta 5 za kijeshi hatari na zenye uwezo mkubwa duniani

Image: GOOGLE

Majeshi mengi makubwa duniani yamekuwa yakishuhudia maendeleo ya helikopta za kijeshi za mashambulizi tangu miaka ya 1940s, ingawa ilikuwa mwishoni mwa miaka ya 1960s, ndege hizo zilipoanza kupata uwekezaji mkubwa na kuonekana kama kitu cha lazima mpaka kufikia muongo wa mwisho wa vita baridi.

Helikopta za kijeshi ni moja ya ndege tata za aina yake na ghali zaidi kuzitengeneza, kiasi hata majeshi makubwa duniani kufanikiwa kumiliki helikopta chache tu, huku mengine yakiwa hayana kabisa. Helkopta hizi za mashambulizi zilishuhudiwa kwa mara ya kwanza zikitumiwa na Soviet na operesheni za Serikali ya Afghanistan, ambapo Mi-24 ilipata heshima yake na kutazamwa kama moja ya zana hatari iliyotumiwa na wapiganaji wa kiislamu.

Helikopta hizi za kushambulia zilitumiwa na pande mbili kwenye vita vya Iran-na Iraq, iliyokwenda sambamba na vita huko Afghanistan na kushuhudiwa vita vikubwa zaidi kuwahi kupiganwa vilivyohusisha mashambulizi ya helikopta.

Kutokana na umuhimu na nguvu zake kwenye vita, ifuatayo ni orodha ya helkopta 5 za kijeshi zenye uwezo na nguvu zaidi za kushambulia, kwa mujibu wa mtandao wa military watch magazine .

Ka-52 Alligator

Image: GETTY IMAGES

Moja ya aina za helikopta zenye nguvu kubwa ya kushambulia kuwahi kutengenezwa tangu kumalizika kwa Vita Baridi, Ka-52 ilianza utengenezaji wa ndege hizo mnamo 2008 na inakadiriwa kuwa ziko helikopta 155 kwa sasa zinazotumiwa na Jeshi la Urusi.

Helikopta hizi ni ghali ukilinganisha na helikopta zingine zinazotumiwa na Warusi, na watengenezaji wamedhibiti uuzaji na usambazaji wake, huku Misri ikiwa mteja pekee ikiwa na aina hizo za ndege 46.

Ka-52 zina ufanisi mkubwa wa kulenga, ikitumia injini zinazofanana na helikopta zingine lakini ikiwa na sauti ndogo inapokatiza ama kupita karibu yako. Ina uwezo wa kubeba mizinga mikubwa ukiwemo wa Kh-31 wenye uwezo wa kushambulia umbali wa zaidi ya kilometa 1300km (Umbali wa kutoka Zanzibar mpaka Mwanza, Tanzania au kutoka Mombasa, Kenya mpaka Juba, Sudan Kusini.

Mi-28NM Havoc

Image: MILLITARYWATCH

Urusi ni nchi pekee inayotengeneza helikopta kubwa na zenye nguvu za kushumbulia zaidi ya moja, ukiacha Ka-52, helikopta za Mi-28 ni moja ya zana zake ghali zaidi ikizidiwa kidogo na alligator.

Helikopta hizi zimekuwa zikitoa huduma tangu mwaka 2009 , na zimekuwa zikiuzwa katika nchi za Algeria na Iraq . Kuhusu uwezo wake, nguvu , kudumu kwake na urahisi wa kurekebisha inapopata shida ya kiufundi, Mi-28 inaonekana bora kuliko Apache, helikopta za Marekani ambazo zinaokena kukaribiana kiushindani na Mi-28.

Mi-28NM, moja ya toleo la aina hizi za helikopta ilipelekwa kufanya operesheni ya kijeshi huko Syria mwaka 2017, na kwa sababu ya ufanisi wake, wizara ya ulinzi ya Urusi imesaini mkataba wa kupeleka helikopta 98 zaidi mpaka kufikia mwaka 2027.

AH-64E Apache

Image: AVIATIONIST

Kufuatia ndege yake ya kwanza mwaka 1975, Helikopta ya kijeshi ya AH-64 Apache ilipitia wakati mgumu mpaka ilivyokuwa tayari kufanya kazi ama kutumia miaka 11 baadae. Awali helikopta hizi zilitengenezwa kwa malengo ya kutoa msadaa wa kushambulia dhidi ya vifaru vya maadui , ikitajwa kuwa na nguvu na nzuri zaidi kuliko helkopta ya AH-1 Cobra na ina uwezo wa kubeba silaha zenye nguvu.

Mi-24P/Mi-35 Hind

Image: GOOGLE

Ikianza kutoa huduma kuanzia mwaka 1972, Mi-24 Hind inachukuliwa kama helikopta ya kutisha zaidi ya tangu enzi ya vita baridi na imethibitisha kuwa na uwezo mkubwa katika mazingira mengi. Ingawa zilizokuja kutengenezwa baada ya vita baridi , hazikuwa na nguvu sana ukilinganisha na Apache, lakini bado zinatajwa kama moja ya helikopta bora ya aina yake, huku toleo la kisasa la Mi-24P ikionekana kuendesha mashambulizi makali dhidi ya waasi wenye silaha huko Syria.

Hind ni helikopta inayopendwa zaidi ulimwenguni ikiwa na tofauti kubwa ya viwango na zingine, ina waendeshaji karibu 60 wanaoendesha, ukilinganisha na 17 wanaopendelea na kuendesha Apache na wawili kwa Mi-28.

Z-10M

Image: GOOGLE

Helikopta za kijeshi zinazofanya mashambulizi ya kijeshi zinabaki kuwa moja wapo ya uwanja ambao sekta ya ulinzi ya China bado iko nyuma ukilinganisha na wenzao wa Marekani na Urusi. Helikopta yake ya Z-10 ikiwa na uwezo mdogo kuliko Apache au haina muundo wa kisasa kama za Urusi lakini imeshuhudiwa maboresho makubwa kwa utendaji wake tangu ilipoanza kutoa huduma. Faida kubwa iliyonayo Z-10 ukilinganisha na helikopta zingine za washindani wake ni kwamba, yenyewe ni rahisi kuifanyia marekebisho inapopata hitilafu, uendeshaji wake unatumia gharama kidogo ukilinganisha na zingine na inapatikana kwa wingi, jambo ambalo linaweza kuwa muhimu na viwango vya juu vya upatikanaji, ambavyo vinaweza kuwa muhimu zaidi wakati pengo la uwezo na utendaji wa helikopta hizo na zile za mahasimu wao likizidi kupungu.