Elgiva Bwire, gaidi aliyeingiza gruneti uwanjani Nyayo siku ya mashujaa

Muhtasari

• Gaidi aliyetoweka Elgiva Bwire Oliacha almaarufu Seif Deen Mohamed almaarufu Japhar almaarufu Japhel Okuku almaarufu Abu Muadh alikuwa kwenye darubini ya pilosi kabla ya kukamatwa Novemba 2011.

Elgiva Bwire alizua tumbo joto miongoni mwa maafisa wa usalama mwaka wa 2011 baada ya kujipenyeza na guruneti hadi kwenye uwanja uliokuwa umejaa watu.

Gaidi aliyetoweka Elgiva Bwire Oliacha almaarufu Seif Deen Mohamed almaarufu Japhar almaarufu Japhel Okuku almaarufu Abu Muadh alikuwa kwenye darubini ya pilosi kabla ya kukamatwa Novemba 2011.

Hii ilikuwa baada ya familia yake kuripoti kwa polisi kwamba alikuwa ametoweka na alishukiwa kuvuka hadi Somalia kwa mchakato kupata mafunzo ya itikadi kali.

Lakini haikuzua mhemko au wasiwasi mwingi alipotoweka Februari 2010.

Ilikuwa hadi siku ya Mashujaa Oktoba 20, 2011, alipokutana na mamake Jacinta Bwire katika uwanja wa Nyayo.

Katika uwanja huo, alikuwa amebeba guruneti lililofunikwa kwenye beseni iliojaa peremende.

Alikuwa amebeba guruneti moja hadi Uwanja wa Nyayo "kwa majaribio."

Katika uwanja huo, alikuwa amejifanya mchuuzi akiuza peremende.

Polisi walikuja baadaye wakapata gruneti walipofanya msako nyumbani kwake.

Elgiva aliwaambia polisi kuwa alienda uwanjani na kuchanganyika na wananchi waliofika kwa hafla hiyo iliyoongozwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki chini ya ulinzi mkali.

Vyombo vya usalama vilikuwa na hofu ya kutekelezwa kwa mashambulizi lakini havikujua mshambuliaji alikuwa Elgiva ambaye alijifanya kama mchuuzi na kupita kwenye mitego yao.

Aliamua kutolipua kilipuzi hicho kwa sababu ya mvua na pia kukutana na mamake kulimvuruga akili.

Jacinta aliwaambia polisi kwamba alikuwa amekutana na mwawe baada ya karibu mwaka mmoja alipokuwa akitoka nje ya uwanja.

Elgiva aliondoka uwanjani akiwa na shehena yake hatari na kwenda nyumbani kwake, ambamo hakukuwa na samani hata moja, isipokuwa mkeka wa maombi.

Jacinta alisema hiyo ilikuwa mara ya kwanza alikuwa akikutana na mwanawe tangu mwezi Februari 2010.

Alisema Elgiva, ambaye ni mtoto wa Jacinta wa tatu kati ya watoto watano, alimwambia wakati huo kwamba alikuwa Mombasa na alikuwa amerejea Nairobi mnamo Agosti 2011.

Alikiri kuwa gaidi

Baada ya kukamatwa, alikiri kuwa gaidi na mwanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.

 Elgiva alihudhuria shule ya msingi mtaani Dandora na kutoweka nyumbani mnamo Februari 2010 hadi mwaka mmoja baadaye. 

Alikuwa ameenda Somalia ambako alipokea mafunzo ya itikadi kali. Alisema kisha alipokea maagizo kupitia barua pepe iliyomwambia achukue mzigo kutoka Eastleigh, Nairobi. Ndani yake kulikuwa na gruneti 20 na risasi.

Haijabainika jinsi shehena hiyo ilisafirishwa hadi Eastleigh lakini maafisa wanaofahamu walisema waliwatafuta na kuwanasa wote waliohusika katika mchakato huo. Elgiva baadaye alisema alitumia guruneti saba kabla ya kunaswa. 

Ajabu ni kwamba alikuwa amechapisha ujumbe kwenye mtandao wa Facebook akitumia ukurasa wake rasmi akisema angeshambulia maeneo 13 zaidi kabla ya kukamatwa. 

Hajapatikana tangu Oktoba 28 baada ya kuachiliwa kutoka kwa Gereza la Kamiti Maximum. Alikuwa amefungwa maisha lakini alikata rufaa na kupunguzwa hadi miaka 10, ambayo alitumikia na akamaliza. 

Wakili wake na msomi wa Kiislamu Prof Hassan Nandwa pia alitekwa nyara na kuachiliwa baada ya siku 10 mikononi mwa watekaji wake. 

Baadaye alikataa kuzungumzia suala hilo. Polisi walidai walipokea ripoti kwamba Elgiva aliwaahidi marafiki zake wa zamani ambao wanatumikia mashtaka mbalimbali ya ugaidi katika Gereza la Kamiti kwamba atafanya shambulio ili kuwaachilia huru mara tu baada yake kuachiliwa. 

Polisi wanasema wanashuku kuwa alijiunga tena na seli ya magaidi, ambao alikuwa akiwasiliana nayo akiwa katika Gereza la Kamiti.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO