Siasa za Kenya, vijana wataka siasa za sera

Muhtasari

• Kenya itasonga mbele vijana wakiwa wamehamasishwa na kuinuliwa kiamaisha. Tunahitaji kuenda shule na sio tu kupata bora elimu, bali elimu bora.

• Vijana wengi waliathiriwa na janga la Corona,wengi wetu walipoteza kazi zao, wengine walifukuzwa manyumbani na sasa wamesalia maskwota wakiishi mitaani.

• Kama kuna wakati wa vijana wanafaa kusimama kidete ili wasikilizwe ni sasa.

Huku siasa za mwaka ujao zikipamba moto na kila nuaniaji akizuru maeneo mbali mabli kuuza sera zake kwa wakenya, kuna jambo moja haswa limewekwa pembeni.

Vijana ambao ndio wengi nchini wametupiliwa mbali sana . Kila sera ni kuhusu uchumi ubora wa maisha na kuendeleza Kenya, mambo yote ya muhimu, lakini vijana ambao ni nguzo muhimu katika ujenzi wa nchi wamewekwa katika kaburi la sahau.

Miaka nenda miaka rudi vijana tumetumika vibaya na wanasiasa,kutoka kuanzisha vurugu na hata kura zetu kununuliwa kwa pesa. Wanasiasa kwa muda wameonelea ya kwamba vijana ni watu wa kupewa fedha ili wajitokeze kupigia kura waliowapa pesa. Jambo ambalo tumeanza kuona miongoni mwao, zaitwa kiunua mgongo au hand-outs ukipenda.

Kenya itasonga mbele vijana wakiwa wamehamasishwa na kuinuliwa kiamaisha. Tunahitaji kuenda shule na sio tu kupata bora elimu, bali elimu bora.

Bado sijiaskia kuhusu sera za kufanya elimu iwe bora kwa wale wasiojiweza au kutoka familia fukara. Vyuo zetu vinadorora kila uchao, kielimu Kenya hatupo tulipokuwa miaka iliyopita . Wanasiasa wanapokuja kwenye vyuo vyetu hakuna cha maana wanachosema kuendeleza taasisi za elimu ila kuuza sera zao kuhusu manufaa yao ya kibinafsi katika siasa.

Wanakuja vyuoni kugawa pesa na kununua kura za vijana wetu. Huku miundo mbinu yetu ya elimu ikiwa imeharibika kiasi cha kutorebikika. Vyuo vingine vimefungwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kuziendeleza, huku wanasiasa wakisaka tu kura za hao vijana ambao sasa hawana be wala te . Wanataka kuunda nafasi za kazi , lakini nani atafanya kazi hizi kama hatuna kisomo.

Vijana wengi waliathiriwa na janga la Corona,wengi wetu walipoteza kazi zao, wengine walifukuzwa manyumbani na sasa wamesalia maskwota wakiishi mitaani. Mambo kama haya sijaskia yakizungumziwa na wanasiasa kwani kwao si ya maana kura ndio za maana kwao ili wajipe mamlaka.

Kijana kama huyu aliyepoteza kazi atafanyia nini wheelbarrow akipewa au akipewa 6,000 kila mwezi, fedha hizi hata atazipata aje. Tunahitaji sera nzuri kuliko wanazotupa hawa wanasisa. Tunahitaji idara itakayo shughulikia wote waliopoteza kazi na kubaini nafasi za kazi zilizopo na namna ya kuunda nafasi za kazi.

Tumechoshwa na kupewa kazi za sulubu kila uchao ambazo baada ya muda mfupi zinakatika na tunarejea pale pale tulipokuwa. Pesa hata tunaambiwa zitatoka baada ya mwezi, twala nini mwezi mzima. Mradi wa kazi kwa vijana ulitupiliwa mbali huku wazee waliokula chumvi wakipewa kazi kila uchao na serikali.

Kama kuna wakati wa vijana wanafaa kusimama kidete ili wasikilizwe ni sasa. Tuko tayari kukaa chini na kusikilizana na mwanasiasa yeyote aliye na sera za kutupeleka mbele. Tumechoshwa na mikutano ya hadhara ya kutuambia tu kuhusu yaliyopita na mabaya kuhusu mpinzani wako.

Tunataka vikao kusikilizwa na maslahi yetu kuzingatiwa. Wakati unabadilika wakenya haswa vijana wamechoka kufanya mambo yale yale nah ii ndio sababu wengi hata hawataki kujisajili kama wapiga kura. Wakati wa mwamko mpya umewadia.

Mahariri: Davis Ojiambo