Baadhi ya watu mashuhuri walioaga dunia mwaka wa 2021

Muhtasari

•Tutu ambaye alisifiwa sana kwa kuhusika katika harakati dhidi ya utawala wa wazungu walio wachache aliaga akiwa na umri wa miaka 90 baada ya kupambana na saratani ya tezi dume kwa takriban miaka 20.

Askofu Mkuu Desmond Tutu, Chris Kirubi, John Magufuli
Askofu Mkuu Desmond Tutu, Chris Kirubi, John Magufuli
Image: HISANI

Imesalia siku chache tu tufungue kupungie kwaheri mwaka wa 2021 na tufungue kalenda mpya ya 2022.

Mwaka wa 2021 umekuwa panda shuka zake si haba haswa ikizingatiwa ulikuwa mwaka wa pili tangu janga la Corona lishambulie dunia.

Kumekuwa na mambo kadhaa ya kusherehekea na vile vile mengi ya kuvunja mioyo yametendeka. Wengi wamezaliwa na vilevile tumeomboleza wengi.

Katika makala haya tutaangazia baadhi ya watu mashuhuri ambao wamepoteza maisha yao mwaka wa 2021.

1. Askofu mkuu Desmond Tutu

Habari kuhusu kifo cha askofu mkuu Desmond Tutu kutoka Afrika Kusini ziligonga vichwa vya habari siku ya Jumapili, Desemba 26.

Tutu ambaye alisifiwa sana kwa kuhusika katika harakati dhidi ya utawala wa wazungu walio wachache aliaga akiwa na umri wa miaka 90 baada ya kupambana na saratani ya tezi dume kwa takriban miaka 20.

Juhudi za marehemu zilimfanya kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 1984 katika kile kilichoonekana kuwa pingamizi kuu dhidi ya jumuiya ya kimataifa kwa watawala weupe wa Afrika Kusini.

2. John 'Pombe' Magufuli

Rais wa tano wa jamhuri ya Tanzania John Pombe Magufuli alifariki dunia mnamo Machi 17 mwakani baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.

Magufuli ambaye alikuwa anahudumu katika muhula wake wa pili alifariki akiwa na umri wa miaka 61 kufuatia matatizo ya moyo.

Nafasi yake ilijazwa na aliyekuwa naibu wake Bi Samia Suluhu Hassan.

3. Chris Kirubi

Mfanyibiashara mashuhuri Chris Kirubi alifariki mnamo Juni 14 akiwa nyumbani kwake baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.

Bilionea huyo ambaye alikuwa miongoni mwa Waafrika tajiri zaidi aliaga akiwa na umri wa miaka 80.

Kirubi alimiliki makampuni mengi na kuendesha biashara nyingi kiwemo Centum, International House Limited, Bayer East Afrika Limited, Capital Media Limited, HACO Tiger Brands EA n.k.

4. Yusuf Haji

Mwanasiasa mkongwe na ambaye alikuwa seneta wa Garissa Yusuf Haji alipoteza maisha yake mnamo Februari 15 baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.

Mwanasiasa huyo alikuwa mwenyekiti wa jopo kazi la BBI  na aliwahi kuhudumu kama waziri wa Ulinzi chini ya utawala  wa rais wa zamani Mwai Kibaki .

5.  Naushad Merali

Mfanyibiashara mashuhuri na ambaye alikuwa mwenyekiti wa Sameer Group Naushad Merali aliaga dunia mnamo Julai 3, 2021.

Naushad ambaye aliorodheshwa miongoni mwa Wakenya tajiri zaidi aliaga akiwa na umri wa miaka 70.

6. Orie Rogo Manduli

Mwanasiasa wa zamani Orie Rogo Manduli aliaga dunia mnamo Septemba 20 akiwa nyumbani kwake katika mtaa wa Riverside Drive, Nairobi.

Balozi huyo ambaye alitambulika sana kutokana na mtindo wake wa kipekee wa mavazi alifariki akiwa na umri wa miaka 73 baada ya kuugua kwa muda.

7. Paul Koinange

Aliyekuwa mbunge wa Kiambaa Paul Koinange alifariki mnamo Machi 31 mwakani.

Mbunge huyo alifariki kutokana na maradhi ya Covid-19 alipokuwa akipokea matibabu katika Nairobi Hospitali.

8. Francis Munyua 'Wakapee'

Aliyekuwa mbunge wa Juja Francis Munyua almaarufu kama Wakapee aliaga dunia mnamo Februari 22 mwakani baada ya kuugua saratani ya ubongo kwa kipindi kirefu.