Ripoti ya skendo ambazo zilivuma mwaka wa 2021

Muhtasari

•Tulishuhudia mambo mengi mwaka uliopita ikiwemo mambo ya ajabu, ya kufurahisha, ya kusikitisha na mengine ya kuburudisha.

Profesa Hamo, Karen Nyamu, Kabi wa Jesus
Profesa Hamo, Karen Nyamu, Kabi wa Jesus
Image: INSTAGRAM

Hatimaye tumeufunga mwaka wa 2021 na kufungua kalenda mpya ya 2022.

Tulishuhudia mambo mengi mwaka uliopita ikiwemo mambo ya ajabu, ya kufurahisha, ya kusikitisha na mengine ya kuburudisha.

Katika makala haya tutaangazia baadhi ya kashfa (scandals) ambazo zilivuma sana mitandaoni mwaka wa 2021

1. Kabi aanikwa kama baba asiyewajibika

Mnamo mwezi Januari mwaka jana, madai kwamba mwanavlogu na mtumbuizaji mashuhuri Peter Kabi almaarufu kama Kabi Wajesus alikuwa ametelekeza binti yake yalienea kote mitandaoni.

Picha ya zamani ambayo alikuwa amepigwa pamoja na mwanadada aliyekuwa ameshika mtoto ilienezwa mitandaoni ikidaiwa kuwa mtoto aliyekuwa pichani ni bintiye.

Kabi alishirikiana na mkewe Milly Wajesus kupuuzilia mbali madai hayo huku akieleza kwamba mwanadada aliyekuwa pichani ni binamu yake Shiku na mtoto yule alikuwa mpwa wake.

Licha ya hayo wanamitandao hawakusita kufuatilia suala hilo na ikamlazimu Kabi kufanya vipimo vya DNA kubaini ukweli.

Mnamo mwezi Mei mwanavlogu huyo alijitokeza kukiri kwamba ni kweli yeye ndiye baba wa mtoto huyo. Kabi alisema vipimo vya DNA vilifichua kwamba alimpachika binamu yake ujauzito mnamo mwaka wa 2013.

Kabi aliomba familia na mashabiki wake msamaha kwa yote yaliyokuwa yametendeka huku akiahidi kuwajibikia bintiye.

2. Drama za Karen Nyamu na Samidoh

Wakili na mwanasiasa mashuhuri Karen Nyamu amekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanamuziki Samuel Muchoki almaarufu kama Samidoh kwa kipindi kirefu licha ya nyota huyo wa Mugithi kuwa na mke na watoto wawili.

Mwaka wa 2020 mahusiano kati yao yalikuja kufumbuliwa ila kwa wakati huo Samidoh akajitokeza kupuuzilia madai hayo.

Hata hivyo mnamo mwezi Februari mwaka uliopita Bi Karen Nyamu aliweka wazi mahusiano yao na kufichua kwamba staa huyo wa Mugithi ndiye baba mzazi wa mwanawe, Sam Juniour.

Karen hakupendezwa na suala la Samidoh kuficha ukweli kuhusu mahusiano yao na kuweka mtoto wao kama siri ndiposa akashinikizwa kumwaya mtama.

Mnamo mwezi Machi Samidoh alithibitisha kwamba alikuwa ametoka nje ya ndoa na kujitosa kwenye mahusiano na mwanasiasa huyo, jambo ambalo lilipelekea kuzaliwa kwa mtoto wa kiume.

Samidoh aliomba familia na mashabiki wake msamaha na kuahidi kuwajibikia watoto wake wote bila kubagua.

Wawili hao wameendelea na mahusiano yao ya kando na hata wanatarajia mtoto wa pili hivi karibuni.

3. Prof Hamo na Jemutai

Wachekeshaji mashuhuri Herman Kago (Prof Hamo) na Stella Bunei Koitie (Jemutai)  wamekuwa wakichumbiana kwa kipindi kirefu.

Mahusiano yao hata hivyo yalikuwa siri hadi mapema mwaka huu mwisho wa mwezi Aprili wakati ambapo Jemutai alimfichua Hamo kama baba asiyewajibika.

Jemutai alidai kwamba mchekeshaji huyo mwenzake alikuwa ametelekeza watoto wao wawili kwa kipindi kirefu. Alisema kwamba Hamo hakuwajibikia watoto wake hata kidogo.

Mapema mwezi Mei Hamo kupitia ukurasa wake wa Instagram akisema amekuwa akiwahudumia watoto wake tangu siku ya kwanza na hakuna siku walikosa mahitaji muhimu.

Hali ya vuta nikuvute baina ya wapenzi hao wawili ilijitokeza na ilichukua kuingilia kati kwa wasanii wenzao wakiongozwa na Churchill kuwepo na mapatano.

Wawili hao waliweza kusameheana na kwa sasa mahusiano yao sio siri tena kwani Hamo tayari amemkubali Jemutai kama mke wake wa pili.

4. Jacque Maribe amfichua Eric Omondi kama baba asiyewajibika

Mnamo mwezi Oktoba na Novemba mwaka uliopita mchekeshaji Eric Omondi na mtangazaji Jacque Maribe walitumbuiza Wakenya na drama telel kwa kipindi cha wiki kadhaa.

Sarakasi zilianza wakatie Bi Maribe alijitokeza kudai kwamba Omondi hakuwahi anawajibikia mtoto wao wa kiume.

Maribe alidai kwamba aligharamia malezi ya mwanawe pekee yake bila usaidizi wa Omondi ambaye ni baba ya mtoto wake .

Eric alionekana kukerwa na hatua ya Maribe na akaamua kuenda hatua zaidi na kuagiza vipimo vya DNA huku akidai alikuwa na shaka kuhusiana na uzazi wa mvulana huyo. Alisema alishuku kuwa yeye sio baba mzazi wa mtoto wa Maribe akidai kuwa walishiriki mapenzi mara moja tu na walitumia kinga.

Baada ya vuta nikuvute ya kipindi kirefu wawili hao walipatanishwa na Simon Kabu na wakakubaliana kumaliza ugomvi wao.

5. Diana Marua vs Willy Paul

Mnamo mwezi Desemba mke wa Bahati alijitokeza kudai kwamba Willy Paul aliwahi kujaribu kumbaka miaka kadhaa iliyopita.

Diana alitengeza video akieleza yaliyotokea kati yake na mwanamuziki huyo ambaye kwa miaka mingi amekuwa akizozana na mume wake Bahati.

Willy Paul hata hivyo alipuuzili mbali madai hayo na hata kupeleka malalamihi mahakamani.