Wafahamu watangazaji wa zamani waliogeuka kuwa wanasiasa maarufu nchini Kenya

Muhtasari

•Katika makala haya tutaangazia baadhi ya wanahabari wa zamani ambao waliwahi kujitosa siasani na kufanikiwa

Rapahel Tuju, Mohammed Ali, Sabina Chege
Rapahel Tuju, Mohammed Ali, Sabina Chege
Image: HISANI

Hatimaye tumeingia mwaka wa siasa. Mwaka wa 2022 unatarajiwa kuwa mwaka wa shughuli nyingi hapa nchini Kenya kwani kampeni za chaguzi za mwezi Agosti zinatarajiwa kushika kasi.

Watu wengi wamejitosa kwenye siasa. Wasanii, wanahabari, wachezaji, mawakili ni baadhi ya wataalamu ambao wamevutiwa na viti vya kisiasa.

Katika makala haya tutaangazia baadhi ya wanahabari wa zamani ambao waliwahi kujitosa siasani na kufanikiwa. Angalau wanasiasa 7 wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali kwa sasa waliwahi kuwa waandishi wa habari.

Raphael Tuju - Katibu Mkuu Jubilee

Katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju, aliingia siasani mwakani 2002 baada ya kuchaguliwa kama mbuge wa Rarienda.

Tuju alianza taaluma ya uadishi wa habari zaidi ya miaka thelathini iliyopita. Aliwahi kuwa mtangazaji wa habari katika stesheni ya runinga ya KTN na mwandishi wa gazeti ya Standard.

Kando na hayo, Tuju alikuwa mtengenezaji vipindi za runinga na aliwahi hudumu kwenye ofisi za mawasiliano za mashirika mbali mbali.

Mohammed Ali(Jicho Pevu)- Mbunge Nyali

Raila Odinga, Mohammed Ali
Raila Odinga, Mohammed Ali
Image: FACEBOOK

Wengi walimtambua mbunge wa sasa wa Nyali kutokana na filamu za upelelezi za 'Jicho Pevu'. Ali alitambulika kwa uandishi wa habari za kina za uchunguzi akifanyia kazi stesheni ya KTN.

Kabla ya kujiunga na KTN, Ali alifanya kazi katika stesheni za KBC,Pwani FM, Radio Salaam.Ali alichaguliwa kama mbunge wa Nyali mwaka wa 2017 kwa tikiti ya kibinafsi baada ya kukosa tikiti ya chama cha ODM.

Sabina Wanjiru Chege - Mwakilishi wa Wanawake, Murang'a

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Murang'a alitambulika kama malkia wa redio ya lugha ya Kikuyu.

Sabina ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya afya bungeni aliwahi kuwa mtangazaji katika stesheni za Coro FM na Kameme FM zinazopeperusha vipindi kwa lugha ya Kikuyu pamoja na KBC.

Sabina pia alicheza katika kipindi cha Tausi kilichoonyeshwa kwenye runinga ya runinga ya KBC.

Aliingia siasani mwaka wa 2013 baada ya kushinda kiti cha mwakilishi wa wamama katika Kaunti ya Muranga. Alishinda kiti hicho tena kwenye chaguzi za 2017.

Gathoni Wamuchomba - Mwakilishi wa wanawake, Kiambu

Gathoni Wa Muchomba
Gathoni Wa Muchomba
Image: FACEBOOK

Kama mwenzake Sabina Chege, mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kiambu alihudumu kama mtangazaji wa redio ya Kikuyu hadi mwaka wa 2017 aliponyakua kiti hicho.

Gathoni alikuwa amewania kiti cha ubunge cha Maragua mwaka wa 2007 ingawa hakufanikiwa kukipata.Kabla ya kuchaguliwa, Gathoni alikuwa mtangazaji katika stesheni ya iNOORO FM.

Aliwahi hudumu katika stesheni ya KBC. Gathoni anamiliki stesheni ya televisheni ya UTUGI TV ambayo inawalenga wakulima.

Granton Samboja - Gavana , Taita Taveta

Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja alianza kama mtangazaji akifanya na kampuni ya Royal Media Services .

Inaaminika kuwa Samboja alisaidia kuzinduliwa kwa stesheni ya Radio Citizen.Baadae Samboja aligura Royal Media na kuanzisha stesheni yake ya Radio kwa jina Milele FM kabla ya kuiuza kwa kampuni ya MediaMax mwakani 2012.

Samboja aliacha kazi katika ulingo wa uanahabari mwakani 2017 na kuwania kiti cha ugavana ambacho alifanikiwa kupata. Anahudumu kwa muhula wake wa kwanza.

Naisula Lessuda- Mbunge, Samburu Magharibi

Neisula Lesuda
Neisula Lesuda
Image: FACEBOOK

Mbunge wa Samburu, Naisula Lessuda ambaye pia ni mwanaharakati alihudumu kama mwanahabari katika stesheni ya KBC kwa niaka mingi kabla ya kujiunga na siasa.

Naisula alibahatika kuteuliwa katika bunge la Seneti mwakani 2013 na chama cha TNA baada ya kushirikishwa sana kwenye kampeni.

Kwenye uchaguzi wa 2017, Naisula aliwania kiti cha ubunge cha Samburu Magharibi na tikiti ya chama cha KANU na kufanikiwa ushindi.