Watu 265 wamefariki katika ajali za barabarani mwezi huu, Polisi wasema

Mwendo wa kasi umekuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi za barabarani.

Muhtasari

•Watembea kwa miguu wamechangia vifo vingi, huku Nairobi ikiongoza kwa waathiriwa 85, ikifuatiwa na eneo la Magharibi ambalo linaongoza kwa ajali za pikipiki.

•Omari ametoa wito kwa madereva wa magari kuchukua tahadhari zaidi barabarani huku akiongeza kuwa nchi inapoteza watu wengi katika ajali.

Ajali
Ajali
Image: HISANI

Takriban watu 265 wamefariki katika ajali tofauti za barabara hapa nchini tangu Januari 1, 2022.

Hili ni ongezeko la asilimia 32 ya matukio kama hayo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Kamanda wa trafiki jijini Nairobi Mary Omari amesema takriban watu 201 walifariki kutokana na ajali katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Watembea kwa miguu wamechangia vifo vingi, huku Nairobi ikiongoza kwa waathiriwa 85, ikifuatiwa na eneo la Magharibi ambalo linaongoza kwa ajali za pikipiki.

Zaidi ya watu 400 wanauguza majeraha nchini kutokana na ajali tofauti.

Kisa cha hivi punde kilitokea katika kaunti ya Homa Bay, ambapo trela iliyokuwa ikisafirisha miwa ilipinduka na kuangukia wanafamilia watatu.

Omari ametoa wito kwa madereva wa magari kuchukua tahadhari zaidi barabarani huku akiongeza kuwa nchi inapoteza watu wengi katika ajali.

"Usalama katika barabara zetu unasalia kuwa suala la wasiwasi mkubwa kwa serikali na umma kwa ujumla. Tunapoteza watu wetu wengi kwenye ajali za barabarani, na hivyo kuacha kaya nyingi bila mtu wa kulisha watoto na watoto yatima,” Omari alisema

Kwa mujibu wa polisi, mwendo wa kasi umekuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi za barabarani.

Kuendesha gari kwa vibaya, kupita magari mengine kwa njia hatari, kuendesha gari ukiwa mlevi, kutembea ukiwa mlevi, kukosa kutumia helmeti, miongoni mwa masuala mengine, pia yamechangia katika ongezeko la ajali.