"Walikuwa watoto wazuri!" Mama ya ndugu waliouawa Kitengela mwaka jana awakumbuka wanawe

Muhtasari

•Bi Wanjiru aliwakumbuka wanawe Fredrick Muriithi na Victor Mwangi kama vijana waliokuwa na maadili mema.

•Wanjiru alisema wakati alipokuwa nchini Uingereza aliwasiliana na wanawe kila siku na aliendelea kuwapa ushauri wa kimaisha.

Bi Lucy Wanjiru aliyepoteza wanawe wawili Kitengela
Bi Lucy Wanjiru aliyepoteza wanawe wawili Kitengela
Image: RADIO JAMBO

Mama ya ndugu wawili ambao waliuawa katika eneo la Kitengela mnamo mwezi Agosti mwaka jana, Bi Lucy Wanjiru angali anawaomboleza watoto wake.

Akiwa kwenye mahojiano na Lynn Ngugi, Bi Wanjiru aliwakumbuka wanawe Fredrick Muriithi na Victor Mwangi kama vijana waliokuwa na maadili mema.

Wanjiru alisema aliwalea wanawe pekee yake na kuwapa mafunzo mema baada ya kutengana na aliyekuwa mume wake zaidi ya miongo miwili iliyopita.

"Nimekuwa na wao vizuri. Niliwalea pekee yangu. Nilikuwa nimeolewa miaka mingi iliyopita na  tukatalikiana na mume wangu mwaka wa 2000. Ilikuwa mzozo wa kinyumbani, hata FIDA walinisaidia kutoka kwa boma hiyo. Tulipelekana kortini na mwanamume huyo akaagizwa akae mbali nami. Alienda njia zangu nami nikabaki na watoto. Kuanzia hapo nilianza kuwalea pekee yangu" Bi Wanjiru alisema.

Alieleza kwamba aliwalea watoto wake kutumia mapato ambayo alipata kutokana na biashara ambazo alijihusisha nazo.

Wanjiru alisema wanawe walikuwa na tabia tofauti ila wote walikuwa na maadili mema na alijivunia kuwa nao.

"Fred alikuwa mwaminifu sana. Alikuwa mtu mtiifu. Ni mtu ambaye hangekukasirisha hata kidogo, nadhani mara ya mwisho nilimpiga alikuwa na miaka mitano. Alikuwa mtu wa kunyeyenyekea, hakuta vita ata kidogo. Hata shule hakufukuwahi kufukuzwa hata kidogo hadi akamaliza kidato cha nne. Hata karo ya shule nilikuwa nampatia akalipe mwenyewe" Alisema.

Alifichua kwamba mwanawe wa pili, Victor alikuwa msumbufu kwa kiwango fulani ila pia alikuwa mchangamfu na angeweza kufurahisha mtu kwa urahisi.

"Alikuwa mvulana mkaidi. Hata hivyo alikuwa kijana ambaye baada ya kunikasirisha angenifanya nifurahie haraka sana. Walikuwa watoto wazuri sana" Wanjiru alisema.

Mama huyo alisema kuwa wanawe walikuwa wenye bidii na malengo makubwa na walijitosa kwenye kazi na biashara mbalimbali.

Alisema hata baada yake kuenda kutafuta riziki ughaibuni wanawe waliendelea na kazi zao vizuri na walijitunza vizuri.

"Hakuna watu waaminifu kama hao vijana. Walikuwa waaminifu sana. Hakuna hata shilingi moja yangu walikula. Walikuwa wananiambia  nikumbuke ndoto zake. Nikienda UK niliwaambia nataka nijenge nyumba. Walikuwa vijana wazuri" Wanjiru alisema

Wanjiru alisema wakati alipokuwa nchini Uingereza aliwasiliana na wanawe kila siku na aliendelea kuwapa ushauri wa kimaisha.

Fred na Victor walizikwa mnamo Agosti 20 mwaka jana katika eneo la Nyahururu, kaunti ya Nakuru.