Miradi maalum ambayo hayati Mwai Kibaki atakumbukwa kwayo

Muhtasari

•Hayati atakumbukwa kwa miradi kadhaa mikubwa ambayo alifanikisha katika kipindi cha utawala wake.

Hayati Mwai Kibaki ambaye alifariki Aprili 22, 2022
Hayati Mwai Kibaki ambaye alifariki Aprili 22, 2022
Image: MAKTABA

Siku ya Ijumaa ripoti za kuaga dunia kwa rais wa tatu wa Kenya, Emillio Mwai Kibaki ziligongwa vichwa vya habari kote duniani.

Maelfu ya Wakenya walimwomboleza Kibaki huku wengine wengi wakitumia fursa hiyo kumsherehekea kwa makubwa aliyofanya katika muhula wake wa utawala wa miaka 10.

Kibaki ambaye alitawala kati ya 2002-2013 alifariki akiwa na umri wa miaka 90.

Hayati atakumbukwa kwa miradi kadhaa mikubwa ambayo alifanikisha katika kipindi cha utawala wake.

i) Elimu ya shule ya msingi bila malipo

Kibaki alipotwaa uongozi takriban miongo miwili iliyopita, moja ya mageuzi aliyoleta ni kuondoa malipo ya shule ya msingi.

Hayati alizindua masomo bila malipo katika jitihada za kuhakikisha kwamba watoto wote wamepelekwa shuleni na angalau kupata masomo ya msingi. 

Rais huyo wa zamani alielekeza adhabu kali kwa wazazi ambao walikosa kupeleka watoto wao shuleni licha ya karo kuondolewa.

Mzazi alihitajika tu kununulia mtoto wake sare ya shule, vifaa vya kuandika na chakula. Serikali ya Kibaki iligharamia mengine.

ii) Thika Super Highway

Thika-Road-Jam
Thika-Road-Jam
Image: MAKTABA

Mtu anaposafiri kutoka eneo la Kati mwa Kenya kuelekea  Nairobi  aghalabu atajipata akimkumbuka rais wetu wa tatu Mwai Kibaki.

Barabara kuu ya kutoka Thika kuelekea Nairobi ni mradi wa Kibaki ambao ulitekelezwa katika muhula wake wa pili.

Ujenzi wa Thika Super Highway uling'oa nanga mwaka wa 2009 na kukamilika 2012. Uligharimu takriban shilingi Bilioni 31.

Njia nane zilijengwa kwenye barabara hiyo kuu katika juhudi za kupunguza msongamano wa magari.

Baada ya kifo cha Kibaki baadhi ya Wakenya walipendekeza barabara hiyo ibadilishwe jina kuwa Mwai Kibaki Highway.

iii) Katiba ya 2010

Mwaka wa 2010 rais Kibaki aliongoza nchi ya Kenya kufanya mageuzi kwenye katiba iliyokuwa inatumika hapo awali.

Katiba ya 2010 ilibadilisha katiba ya zamani iliyokuwa ikitumika tangu Kenya ipate uhuru mwaka wa 1963.

Hayati Kibaki ni miongoni mwa viongozi ambao waliipigia debe sana katiba tunayotumia hadi wa sasa.

iv) Vision 2030

Vision 2030 ni mpango wa ukuaji wa nchi ambao ulizinduliwa na rais Kibaki mnamo Juni 10, 2008.

Mpango huo unalenga kubadilisha Kenya kuwa nchi mpya ya kiviwanda na ya kipato cha kati inayotoa maisha bora kwa raia wake wote katika mazingira safi na salama.

Hayati pia atakumbukwa kwa mafanikio mengine makubwa kama ukuzaji wa uchumi wa Kenya na uboreshaji wa hali ya maisha.

Mungu ailaze roho ya Hayati Kibaki mahali pema peponi.