Samuel Muvota: Fahamu mambo ya kutisha usiyoyajua kuhusu jambazi sugu aliyeuawa Kasarani

Muhtasari

•Muvota aliuawa Jumatatu mwendo wa alasiri kwa kupigwa risasi katika mtaa wa Mirema Drive, eneo la Kasarani, kaunti ya Nairobi.

•DCI amewasihi Wakenya kusaidia katika kukamatwa kwa mshukiwa mkuu Denis Karani ambaye inadaiwa huenda tayari amevuka mpaka wa Kenya.

Marehemu Samuel Mugo Muvota
Marehemu Samuel Mugo Muvota
Image: TWITTER// DCI

Samuel Mugoh Muvota amekuwa gumzo ya mtaa na mitandaoni katika kipindi cha takriban siku kadhaa ambazo zimepita.

Hii ni kutokana na mambo ya kutisha ambayo kitengo cha DCI kimekuwa kikifichua kumhusu baada yake kuuawa katika hali tatanishi siku ya Jumatatu.

Muvota aliuawa Jumatatu mwendo wa alasiri kwa kupigwa risasi katika mtaa wa Mirema Drive, eneo la Kasarani, kaunti ya Nairobi.

Marehemu hakutambuliwa mara moja baada ya kuuawa ila siku moja baadae polisi wakafichua kuwa alikuwa na historia kubwa ya uhalifu.

Kitengo cha DCI kimetoa msururu wa maelezo ya kutisha kuhusu maisha ya giza ya Muvota. Katika makala haya tumekusanya maelezo muhimu kuhusu maisha ya Muvota:-

  • Muvota alianza maisha ya uhalifu mwaka wa 2011. Alianza kwa kulaghai watu kisha kuiba kutoka kwenye akaunti zao za benki
  • Kufikia kifo chake alikuwa anamiliki na kusimamia akaunti za benki zaidi ya 300.
  • Mwaka wa 2018 aliwahi kuiba Ksh 800,000 kutoka kwa akaunti ya mwanamke ambaye alizirai na kufariki punde baada ya kugundua kilichofanyika.
  • Amewahi kukamatwa zaidi ya mara 30 katika kipindi cha miaka 11 ambacho kimepita.
  • Kando na kuiba kutoka kwa akaunti za benki za watu, Mugota pia aliibia watu katika maeneo ya burudani kwa kutumia usaidizi wa wanawake wenye sura za kuvutia.
  • Mugota aliajiri zaidi ya wanawake 50 ambao walimsaidia kwa kuweka dawa za kupoteza fahamu kwenye vileo au vyakula vya wanaume kisha kuwaibia.
  • Alikuwa na wake saba ambao wanaishi maisha ya kifahari. Hakuna mke aliyejua kuhusu maisha ya uhalifu ya Muvota.
  • Marehemu ni baba ya watoto wengi ambao idadi yao halisi haijathibitishwa.
  • Aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu asiyejulikana mnamo Mei 16, 2022 katika mtaa wa Mirema, Eneo la Kasarani, Nairobi.
  • Muvota anadaiwa kuuawa na mfanyikazi wake Denis Karani ambaye walizozana naye kuhusu mgao wa biashara yao ya ‘mchele’ na wanawake ambao wamekuwa wakishiriki ngono nao kabla ya kuwaajiri kwenye genge lao la uhalifu.

Siku ya Ijumaa DCI Kinoti alitangaza kuwa baadhi ya wanawake ambao Muvota alikuwa ameajiri katika biashara yake ya kutilia wanaume ‘mchele’ tayari wamekamatwa.

Pia aliwasihi Wakenya kusaidia katika kukamatwa kwa mshukiwa mkuu Denis Karani ambaye inadaiwa huenda tayari amevuka mpaka wa Kenya.