Kahaba aliyegeuka kuwa mchungaji

Muhtasari

• Maisha aliyoishi Jane, yaliendelea kuwa ya mashaka na wakati alipotimiza umri wa miaka 17 alipata ujauzito. ''Nilipata ujauzito wakati nilipokuwa nikiishi na mpenzi wangu'', anasema.

Mchungaji Jane Watere alikuwa Kahaba na mtumiaji sugu wa dawa ya kulevya
Mchungaji Jane Watere alikuwa Kahaba na mtumiaji sugu wa dawa ya kulevya
Image: JANE WATERE

Anajulikana na wengi hasa katika kitongoji chake cha mtaa wa mabanda wa huruma jijini Nairobi nchini Kenya kama Mchungaji Jane Watere. Lakini anapokusimulia maisha yake ya awali unabakia kinywa wazi na kujiuliza ni kwa jinsi gani ameweza kubadilika na kuwa alivyo sasa-Mchungaji wa Kanisa..

Nilipozungumza naye Mchungaji Jane Watere aliniambia kuwa alikuwa Kahaba na mtumiaji sugu wa madawa ya kulevya tangu alipokuwa na umri wa miaka 13 hadi alipofikia umri wa utu uzima.

Jane ana umri wa miaka 42 katika mtaa wa mabanda eneo la Huruma nchini Kenya. Mama huyu aliyejaliwa watoto wawili anakiri kwamba alilelewa na wazazi waliokuwa na upendo na walifanya kila wawezalo kuwapa malezi yenye nidhamu na maadili mema.

Maisha ya ukahaba

Lakini alipoingia umri wa kubalehe alianza kuchukua mkondo tofauti wa maisha kwani anasema hakuona haja ya masomo alipofika darasa la 5 ghafla alikataa masomo.

Kilichofuata ni kumsihi mzazi wake kumpeleka kwenye mafundisho ya ushonaji na wakati mmoja mafunzo ya ususi. Hatahivyo yote haya yalishindikana kwani anasema aijiingiza kwenye hali ya kuwa mlevi wa pombe , uvutaji wa bangi na gundi kama njia ya kujivinjari .

"Masomo yalinishinda nikiwa bado binti mdogo sana , nakumbuka mama yangu akinisihi kusoma ila sikumsikia . Nakumbuka wakati mmoja nikiwa na miaka 16 nilifungwa gerezani kwa muda wa mwezi mmoja kwa kosa la kurandaranda .Ni hivyo maisha yangu yalivyokuwa bila mwelekeo kabisa "anakumbuka Jane

Maisha aliyoishi Jane, yaliendelea kuwa ya mashaka na wakati alipotimiza umri wa miaka 17 alipata ujauzito. ''Nilipata ujauzito wakati nilipokuwa nikiishi na mpenzi wangu'', anasema.

Jane alijaaliwa kupata kifungua mimba ,hatahivyo maisha haya ya ndoa ya utotoni hayakudumu kwani yeye na mpenzi wake waliachana ghafla.

''Tulikuwa katika mapenzi sana na mume wangu, lakini ilishindikana kuishi pamoja na tukatengana na kila mtu akaanza maisha yake mapya''.

Akiwa na umri wa miaka 21 alikuwa hana mume na ni mmoja wa marafiki zake alikuwa amemfahamisha kuhusiana na biashara ya ukahaba ambayo ilikuwa njia rahisi ya kujitafutia riziki .Ila kwa Mchungaji huyo anasema kwamba aliingia kule akitumai kwamba angelipiza kisasi uchungu wa kuachwa katika ndoa yake na mume aliyempenda sana .

"Nakumbuka mara ya kwanza nilipoingia mitaani kuanza kazi hii ya ukahaba , nilikuwa sina ufahamu wa jinsi ya kuvaa, na kwa hiyo siku tatu mfululizo sikuweza kuwapata wateja "anasema Jane

Kulipiza kisasi kwa wateja

katika kazi ya ukahaba wakati wote Jane alikuwa akisumbuliwa na machungu ya ndoa ya kwanza
katika kazi ya ukahaba wakati wote Jane alikuwa akisumbuliwa na machungu ya ndoa ya kwanza
Image: MCHUNGAJI JANE WATERE

Anakiri kwamba maisha ya ukahaba sio mazuri na yamejaa hatari na aibu nyingi mno. Mama huyu anasema kwamba kwa miaka saba aliyofanya kazi hii alikuwa bado na machungu ya ndoa ya kwanza.

Anasema kwamba machungu hayo aliyaelekeza kwa baadhi ya wanaume ambao walikuwa wanahitaji huduma zake .

"Sio mara moja, mbili au hata kumi nilikuwa naandamana na mteja kwenye madunguro, na nisiwe na machungu ya mapenzi ya kale , nilikuwa na tabia ya kuhakikisha kwamba nimeiba nguo za mteja wakati amelala , na baadaye kuzitoa kama zawadi kwa watoto wanaorandaranda mitaani .Matendo hayo ya ajabu niliyafanya bila kujali mteja atatokaje hotelini ", anakumbuka .

Ndoa ya pili

Wakati anafanya kazi ya ukahaba Jane alijipata ameolewa tena kwa mara ya pili
Wakati anafanya kazi ya ukahaba Jane alijipata ameolewa tena kwa mara ya pili
Image: JANE WATERE

Wakati akifanya kazi ya ukahaba alijipata ameolewa tena kwa mara ya pili…ni ndoa ambayo haikukaa kwa muda mrefu kwani anasema kwamba marehemu mume wake alikuwa miongoni mwa magenge ya watu wahalifu.

Baadaye mumewe alipigwa risasi miaka kadhaa iliyopita. Katika ndoa hiyo walikuwa wamejaaliwa mtoto wa kike ambaye sasa ana umri wa miaka 16.

Kutoka kuwa kahaba hadi kuwa mchungaji

Ulimwengu wa ukahaba una misukosuko mingi na visa vya aibu, anakiri mama huyu , ila mahangaiko yote hayo yalikuwa hayamkatishi tamaa ya kila usiku kuwa mitaani au kwenye vilabu vya pombe akiwasaka wateja.

Kubadilika

Jane anasema wakati alipokuwa katika harakati za ukahaba kulikuwa na wahubiri waliokuwa wakifika kwenye baadhi ya maeneo alipokuwa anafanyia kazi hizo , na kwa muda walitenga wakati kumhubiria na vile vile kumuonyesha athari za kushiriki katika ukahaba.

Haikuchukua muda kwa mwanamke huyu kukubali kubadilisha maisha yake alipo enzi dini ya Ukristo na kuokoka.

"Mtaani kwetu watu wanaonifahamu hawakuamini kwamba nilikuwa nimebadilisha maisha yangu , ghafla niliacha kazi za ukahaba na nikaanza kwenda kanisani, kuna wale waliodhani kwamba ni mzaha ila nilikuwa nimemaanisha kubadilika na pia kuanza maisha hasi "Jane anasema.

Jane ( kulia) alifuzu kama Mchungaji baada ya kukamilisha masomo ya theolojia na kuamua kufungua kanisa lake
Jane ( kulia) alifuzu kama Mchungaji baada ya kukamilisha masomo ya theolojia na kuamua kufungua kanisa lake
Image: JANE WATERE

Baada ya kuokoka Jane alianza masomo ya Theolojia katika chuo kimoja nchini Kenya hali kadhalika alikua ameanza hutoa huduma za kutoa nasaha kwa makahaba , wanawake ambao wanatumia mihadarati na pombe kupindukia pamoja na makundi ya vijana wanaoingia kwenye uhalifu mitaani.

Kupitia huduma hizi Jane pia alifuzu kama Mchungaji baada ya kukamilisha masomo ya theolojia na kuamua kufungua kanisa lake lililoko mtaa wa mabanda wa huruma linalojulikana kama Remnants Chosen by God.

Mwanadada huyu amekuwa akihusika sana pia kwa kutoa nasaha kupitia simulizi lake la maisha kama kahaba kama njia ya kuhakikisha kwamba wengi ambao wametekwa kwenye hali hiyo wanapata chaguo lingine la maisha.

Anasema kwamba sio wanawake wote au wanaume ambao ni makahaba wanafanya hivyo kwa kuwa wanafurahia, bali kila mmoja huwa anakuwa na uchungu fulani katika maisha yake unaomsukuma kufanya kazi hiyo.

Hatahivyo anasema iwapo vikundi vya watu wanaojihusisha katika kazi hizo vitapata elimu ya umma mabadiliko yataonekana kwa haraka hasa wanapoonyeshwa upendo na sio unyanyapaa

"Wakati ninatoa simulizi yangu , kumbuka kuwa inatoka kwa mwanamke aliyekuwa amejiingiza ndani ya maadili mabaya na hata uhalifu, lakini sasa mambo ni tofauti mno kwani nimebadilika na kwa kweli ya kale yamepita na sasa ni kiumbe kipya kabisa, najikumbusha kwamba mwanzo wangu hauwezi kuharibu kesho yangu " anasema Jane.