Kufanya kazi katika chumba cha kuhifadhia maiti kulinikausha- Wajackoyah

Muhtasari

•Wajackoyah alilazimika kufanya kazi duni ili kujikimu kimaisha, jambo ambalo limemuunda kuwa kiongozi aliye sasa hivi.

•Alieleza kuwa kazi zisizo za kawaida alizofanya akiwa uhamishoni zilimuandaa kwa ajili ya harakati za ukombozi.

•Alisema alishiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Eritrea, Ethiopia, Angola na hata Kenya

Mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwa Lion's Place kwa mahojiano na Radio Jambo mnamo Juni 10, 2022.
Mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwa Lion's Place kwa mahojiano na Radio Jambo mnamo Juni 10, 2022.
Image: CHARLENE MALWA

Mgombea urais George Wajackoyah amefichua kuwa alifanya kazi kama mhudumu wa chumba cha maiti alipokuwa uhamishoni.

Kiongozi wa chama cha Roots Party of Kenya alisema alilazimika kufanya kazi duni ili kujikimu kimaisha, jambo ambalo limemuunda kuwa kiongozi aliye sasa hivi.

"Kufanya kazi kama mchimba kaburi na mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti kulinipa uwiano ambapo ningeweza kufanya kazi yangu na niliipenda," Wajackoya alisema.

Alienda uhamishoni kutoka 1991 hadi 2012 aliporejea Kenya.

Akiwa uhamishoni nchini Uingereza, mgombe urais huyo alifanya kazi katika hospitali ya Royal free mjini London kama mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti. Makamu wa rais wa zamani Michael Kijana Wamalwa alifariki katika hospitali hiyo mnamo Agosti 23, 2003.

Kabla ya kwenda uhamishoni nchini Uingereza na Marekani, Wajackoyah alifanya kazi kama afisa wa polisi nchini Kenya.

Alieleza kuwa kazi zisizo za kawaida alizofanya akiwa uhamishoni zilimuandaa kwa ajili ya harakati za ukombozi alizoshiriki.

"Kazi zisizo za kawaida nilizofanya ndio jambo bora zaidi lililonipata. Kazi nilizofanya zilinikomaza na kunitayarisha kwa mapambano ya ukombozi,” alibainisha.

Akiwa uhamishoni, alitumia majina kama George Walker kuficha utambulisho wake.

"Ninafichua jina kwa sababu ni zaidi ya miongo mitatu tangu kutokea. Nikiwa huko, nilikaa na watu wasio na makao ili kunifunika nisiwe sehemu rahisi ya madhara hadi ilipokuwa sawa na salama kwangu hata kwenda shule,” Wajackoya alifichua.

Pia alisema alishiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Eritrea, Ethiopia, Angola na hata Kenya.

"Tulitaka kuleta mabadiliko kwa nguvu, kwa meno, kwa mikono. Tulifanya kile tulichotaka kufanya ili kuleta haki.”

Kiongozi wa chama cha Roots Party of Kenya amekuwa msisimko nchini Kenya baada ya kutangaza azma yake ya urais.

Amesema atahalalisha bangi kwa matumizi ya dawa ili kuingiza mapato, pamoja na kutekeleza ufugaji wa nyoka ili kuingiza mapato zaidi ya nchi.

Akiwa na sahihi yake ya kuvaa durag kichwani, Wajackoyah aliidhinishwa na tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka mnamo Juni 2, kuwania urais.

Mwenyekiti Wafula Chebukati alitangaza kuwa Profesa amepata idadi ya wafuasi wanaohitajika kushiriki katika uchaguzi mkuu.

Awali IEBC ilikuwa imekataa ombi la Wajackoyah baada ya kukosa kuweka sahihi 2,000 zinazohitajika kwa kila kaunti katika angalau kaunti 24.

Sasa ameanza kampeni za kutangaza azma yake ya urais kote nchini.

(Utafsiri: Samuel Maina)