Barabara telezi! Jinsi safari ya kisiasa ya Bahati ilivyotatizika

Mgombea ubunge huyo sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Muhtasari

•Safari ya kisiasa ya mgombea ubunge wa Mathare Kelvin 'Bahati' Kioko imekumbwa na misukosuko si haba.

•Katika ujumbe wake wa Jumatatu, mgombea ubunge huyo sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Kevin Bahati
Image: WILFRED NYANGARESI

Safari ya kisiasa ya mgombea ubunge wa Mathare Kelvin 'Bahati' Kioko imekumbwa na misukosuko si haba.

Bahati, 28, alitangaza uingio wake kwenye siasa mnamo Machi 18 mwaka huu ambapo alitangaza azma yake ya kuwania kiti cha ubunge cha Mathare kwa tiketi ya chama tawala cha Jubilee.

Mwishoni mwa Aprili msanii huyo aliidhinishwa na Jubilee na hata kukabidhiwa cheti cha kuwania ubunge na mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho Kanini Kega.

Sijui jinsi ya kusherehekea haya. Sijui nilie au niombe. Hii ni ndoto iliyotimia, sio kwangu tu kama Bahati; bali pia kwa vijana na watu wangu wa Mathare ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiombea mbunge aliyetengenezewa Mathare," Bahati alisema baada ya kupokea cheti hicho.

Siku chache baadae hata hivyo alijitokeza kudai kuwa  cheti alichokuwa amepewa baada ya kushinda katika kura zote za maoni kilikuwa kimebatilishwa.

Aidha alisema aliambiwa ajiuzulu ili kumwachia nafasi mbunge wa sasa Anthony Oluoch, uamuzi ambao hakuwa tayari kufanya.

"Niliambiwa nijiondoe baada ya kupokea cheti cha uteuzi,” alisema na kuongeza kuwa habanduki hata kwa maendeleo hayo mapya.

Hata hivyo, mnamo Mei 13 Bahati aliweza kupumua baada ya chama cha Jubilee kufanya mabadiliko katika uamuzi wake wa kuondoa cheti chake cha uteuzi.

Mwanzoni mwa Juni tume ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) HATIMAYE ilimuidhinisha mwanamuziki huyo kuwania ubunge wa Mathare.

Huku akizungumza baada ya kuidhinishwa Bahati alisema;

"HATIMAYE NIMEIDHISHWA NA IEBC ✅ Asante Mungu, Asante Jubilee Party, Asante Mathare kwa kunikabidhi nafasi hii ya Kuleta Mabadiliko ambayo tumekuwa tukiyatamani... .

Ni Wakati Wa Kubadilisha Uongozi Wetu, Wakati Wa Kupiga Kura Mmoja Wetu. Ni Wakati wa Mathare.

Masaibu hata hivyo hayakuacha kumuandama  Bahati licha ya kuidhinishwa na IEBC.

Kuelekea mwishoni mwa Juni, mgombea ubunge huyo kwa mara ya kwanza alidaiwa kujiondoa kinyang'anyironi na kumuachia mpinzani wake, madai ambayo alijitokeza kutupilia mbali.

“Azimio, acheni kuwapotosha wapiga kura wa Mathare. Bahati - Mathare hajajiuzulu kwa ajili ya mtu yeyote. Puuza propaganda!,” Alitangaza kupitia Instagram.

Takriban wiki mbili zilizopita mwanamuziki huyo alionekana akifukuzwa kutoka kwa mkutano wa Muungano wa Azimio- One Kenya jijini Nairobi. Bahati alilazimika kugura mkutano huo hata kabla ya kuwahutubia wafuasi wake.

Bahati hata hivyo alipuuzilia mbali madai kuwa alifurushwa na kudai kuwa katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna  ndiye aliyekatisha mkutano ghafla baada ya kumuona akiwasili na kundi la wafuasi wake.

Sifuna na Rafiki yake Aliyepoteza uchaguzi mara mingi walipomwona MBUNGE WA MATHARE ANAYEINGIA - BAHATI KIOKO amefika na Umati wa watu ulikuwa Ukitaka kunisikia nikizungumza... Waliamua Kumaliza Mkutano ghafla, kinyume na matakwa ya wananchi wa Mathare,” Alisema

Wikendi mwimbaji huyo alizua drama tena alipogura mkutano wa Azimio baada ya mgombea urais Raila Odinga kumuidhinisha mpinzani wake Antony Oluoch.

Raila akimudhinisha Oluoch aliahidi kumpa Bahati kazi serikalini iwapo atachaguliwa kuwa rais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Baadae Bahati aliweka wazi kuwa hataki kazi hiyo na kumshtumu mpinzani wake Oluoch kwa masaibu yaliyomkumba.

Alitaka ninyang'anywe tiketi nikapewa, upande mwingine akaleta propaganda eti nimejiondoa na nikakataa, akataka nipatiwe kazi nayo pia nimekataa. Leo kwa lazima niwe jasiri na nifanye ninachohitajika kufanya kwa sababu napigania watu wa Mathare.. " Alisema katika video aliyopakia Instagram.

Katika ujumbe wake wa Jumatatu, mgombea ubunge huyo sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarini.