Masaibu ya msichana mwenye maradhi ya uti wa mgongo Naivasha

Clara Waithera familia hiyo ilimpoteza binti mwingine kutokana na maradhi hayo miaka kumi na moja iliyopita

Muhtasari

• Kulingana na stakabadhi kutoka kwa Daktari Fazal Akil kutoka Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), msichana huyo ana ugonjwa hatari na anahitaji upasuaji.

• Scoliosis ni hali ambayo uti wa mgongo hujipinda na kujikunja kwa upande na inaweza kuathiri watu wa umri wowote.

Familia moja eneo la Naivasha inaishi katika hali ya huzuni kufuatia ulemavu ambao ulimpata binti yao miaka kadhaa baada ya mwingine kufariki kutokana na hali hiyo.

Familia ya binti huyo Clara Waithera mwenye umri wa miaka 16 na ambaye ana ulemavu wa uti wa mgongo unaoitwa Scoliosis, inatafuta shilingi milioni nane ili afanyiwe upasuaji kurekebisha hali yake.

Familia hiyo ilimpoteza binti mwingine kutokana na maradhi hayo miaka kumi na moja iliyopita alipokuwa akifanyiwa upasuaji nchini India.

Scoliosis ni hali ambayo uti wa mgongo hujipinda na kujikunja kwa upande na inaweza kuathiri watu wa umri wowote, chanzo bado hakijabainika. Hali hiyo pia inazuia mtoto kukua inavyostahili.

Clara Waithera (katikati) Mamake Nashiku Mwangi na kakake John Kimani.
Clara Waithera (katikati) Mamake Nashiku Mwangi na kakake John Kimani.
Image: ANTONY GITONGA

Kulingana na mamake mzazi Nashiku Mwangi, hali hiyo imeathiri familia kihisia na kifedha kutokana na harakati za kumtafutia binti yao matibabu.

Akizungumza nyumbani kwake mjini Naivasha, Nashiku, alisimulia uchungu wao wakizunguka kutoka hospitali moja hadi nyingine kutafutia matibabu binti yao ambaye ndoto yake ni kuwa daktari.

"Hali hii imeathiri ukuaji wake, ameacha shule, analazimika kulala chini wakati akisoma na ni mdogo sana kwa umri wake," alisema.

Mama huyo wa watoto watatu mwenye hisia kali alisema kuwa bado hajakubali kifo cha mwanawe wa pili na kuongeza kuwa hali ya mtoto wake wa tatu imeacha familia yake katika hali majonzi.

"Binti yangu anahitaji shilingi milioni 8 kwa upasuaji wa haraka nchini India, kiasi ambacho hatuwezi kumudu na tunatumai tutapata usaidizi kutoka kwa watu wema," alisema.

Nashiku alisema walikuwa gizani juu ya chanzo cha hali hiyo kwa mabinti zake wawili na kuongeza kuwa hakuna mtu mwingine katika familia yao aliyekumbwa na hali hiyo.

Kwa upande wake, msichana huyo,Waithera, alikuwa na matumaini kwamba kila kitu kitaenda sawa, akiongeza kuwa kusoma peke yake nyumbani kumeathiri maisha yake.

Alisema kuwa anatazamia kuishi maisha ya kawaida na kuongeza kuwa hali hiyo imemuathiri kimwili na kihisia.

"Dada yangu mkubwa aliaga dunia kutokana na hali hiyo na maombi yangu ni kwamba nitafanyiwa upasuaji wa mafanikio na hatimaye kuwa daktari wa maradhi ya moyo," alisema.

Kaka yao mkubwa John Kimani alisema kuwa hali hiyo imemaliza rasilimali za familia huku wakimtafutia matibabu katika hospitali mbalimbali.

"Bado tunajaribu kukubaliana na uchungu wa kifo cha dada yetu na maombi yetu ni kwamba tupate pesa ili dada yetu mdogo apate matibabu," alisema.

Kulingana na stakabadhi kutoka kwa Daktari Fazal Akil kutoka Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), msichana huyo ana ugonjwa hatari na anahitaji upasuaji.

"Si kawaida kwetu kupata ugonjwa wa Scoliosis kiwango hiki na kwa hivyo napendekeza rufaa nje ya nchi kwa matibabu," alisema katika hati za matibabu.

Nambari ya Paybill ya familia ni 516600, Akaunti 7768968001, Diamond Trust Bank.

 

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO