Watoto wanauzwa wakiwa tumboni, wa kike anauzwa laki 8 na wa kiume milioni moja

Washukiwa hao walisema kuwa wanauza mtoto wa kke kwa laki 8 huku wa kiume akipigwa mnada kwa milioni moja.

Muhtasari

• Sasa hivi kusema ukweli wasichana wametamauka sana, unapata msichana anapata mimba na mwanaume anakimbia" Mandela alieleza sababu ya kina mama kuuza watoto

Washukiwa wa kuuza watoto kimagendo
Washukiwa wa kuuza watoto kimagendo
Image: NTV screengrab, YouTube

Biashara haramu ya uuzaji watoto nchini Kenya imekuwa ikiendelea licha ya serikali na mamlaka mbalimbali kujitahidi kukomesha biashara hiyo ya magendo kwa kuwatia mbaroni washukiwa.

Katika Makala yaliyofanywa na kituo kimoja cha runinga humu nchini, ni hali ya kusikitisha ambayo inasimulia matukio yenye ukakasi jinsi wauguzi katika hospitali moja kaunti ya Kisumu wanashiriki kuwauza watoto kwa watu wanaojiweza.

Katika Makala hayo ya ufichuzi yaliyofanywa kwea njia ya siri, mzalishaji alifanikiwa kukutana ana kwa ana na Steven Odhiambo ambaye ni kiongozi wa genge hilo la biashara haramu ya watoto pamoja pia na Nelson Mandela ambaye ni muuguzi anayefanya kazi katika hospitali ya Ahero.

Makala hayo yalinogeshwa kwa mipango na michakato ya kisiri amabyo ilipangwa kwa kuwatafuta wanandoa feki ambao wangejitambulisha kuwa watu wenye uwezo kutokana na kufanya kazi katika ubalozi mmoja jijini Nairobi na kuwa walikuwa na shida ya mtoto.

Katika kile amabcho hakikutarajiwa kabisa, Mandela alieleza kuwa ni rahisi sana kwa wanandoa hao kupata mtoto kwani wasichana wengi ambao wanapata watoto kabla ya kuolewa wanatamauka sana na ni rahisi kwao kunyang’anywa hao watoto na kuuziwa kwa watu wengine.

“Sasa hivi kusema ukweli wasichana wametamauka sana, unapata msichana anapata mimba na mwanaume anakimbia. Unapata msichana bado ako kwao, hana kitu chochote anafanya, kwa hiyo huwa aghalabu wanatuambia, hata wengine wanakuja tu wanataka kuwauza watoto wao,” tabibu Mandela alieleza.

Kilichoshangaza zaidi ni jinsi wawili hao walikuwa wanapiga mnada watoto utadhani ni mbuzi sokoni ambapo walifunguka kuwa biashara hiyo imewanogea na huwa wanauza watoto kati ya shilingi laki 8 hadi milioni moja kutegemea na jinsia lakini pia kwa vigezo vya yule mwenye hitaji.

Wawili hao walionekana kuwa na uzoefu tayari kwani tabibu Mandela alisema wameshafanikisha kuwauza watoto wawili wachanga mpaka sasa bila tatizo lolote. Mmoja alikuwa ni wa kike ambaye waliuza kwa laki nane na wa kiume akapigwa mnada kwa milioni moja.

Washukiwa hao ambao walikuwa wanafanya biashara kama madalali walikuwa wanamtafuta mwanamke mweney ujauzito na ambaye angependa kumuuza mtoto wake na ingawa walisema wao huuza mtoto kwanzia laki nane, walikuwa wanawambia mama mweney ujauzito kwamba mtoto anauzwa kwa laki moja na nusu ambayo angepewa laki na madalali kubaki na elfu 50. Ukatili ulioje!

Katika kisa kimoja ambacho walimleta mama mjamizto mwenye hitaji la kumuuza mtoto, mama huyo amabye tayari ana watoto wengine alisema kuwa sababu yake kuu kuuza mtoto wake ambaye bado hajazaliwa ni kujikwamua kiuchumi huku madalali hawa wawili wakitoa sababu tofauti kwamba alikuwa amepanga kuondoka kwenye miliki za Kiarabu kwa ajili ya kazi.