GBV:Wabunge wanawake washiriki uzoefu wao, huku wakiadhimisha siku 16 za uharakati wa kijinsia

Buyu alisema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa katika kupambana na tabia hiyo, bado wengi wanateseka kimyakimya.

Muhtasari
  • Naibu Spika Gladys Boss alikumbuka jinsi alilazimika kuajiri wafanyikazi wa usalama wa kibinafsi kumlinda
NAIBU SPIKA GLADYS SHOLLEI
Image: EZEKIEL AMING'A

Idadi ya wabunge wanawake nchini Kenya wameshiriki uzoefu wao wa Unyanyasaji wa Kijinsia (GBV) mikononi mwa wapendwa wao.

Naibu Spika Gladys Boss alikumbuka jinsi alilazimika kuajiri wafanyikazi wa usalama wa kibinafsi kumlinda.

Hii ilikuwa licha ya kuripoti kesi hiyo kwa polisi, ambao hawakutoa msaada wowote.

Akizungumza alipokuwa akiongoza Chama cha Wabunge Wanawake Kenya (KEWOPA) kuadhimisha siku 16 za uharakati wa kijinsia, Boss alishutumu polisi kwa kuhusika katika visa vya GBV.

"Mimi binafsi kama mbunge nimeripoti kwa polisi vurugu nilizofanyiwa, hata nilipopata amri za kuzuia mtu huyo, polisi hawakusaidia, nililazimika kwenda juu zaidi na kuajiri walinzikunisaidia katika usalama wangu” Boss alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Aldai Maryanne Keitany alishiriki tukio ambapo alifurushwa kutoka kwa nyumba yake mnamo 2018, huku polisi wakiwasindikiza waliokuwa wakimfukuza.

Keitany ambaye alipitia kesi kali ya talaka alisema aliumia lakini aliamua kuweka hadharani masaibu yake ili kuwasaidia wanawake wengi ambao walikuwa wakipitia matukio hayo kimyakimya.

“Niliamua kupitia mchakato wa mahakama na nikaiweka hadharani. Watu wengi sana wananifahamu leo, si kwa sababu ya kazi yangu ya awali bali kwa sababu ya kesi hiyo mahakamani, na watu wengi hadi sasa wamezungumza kutokana na uzoefu wangu, kwa sababu ilikuwa kama opera ya sabuni” Alisema Keitany.

Katika hotuba yake, naibu mwenyekiti wa KEWOPA Rosa Buyu aliwataka wabunge kutunga sheria kali ili kuhakikisha uovu huo unang'olewa kutoka kwa jamii.

Buyu alisema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa katika kupambana na tabia hiyo, bado wengi wanateseka kimyakimya.