Usichokifahamu kuhusu mmiliki wa Modern Coast, kampuni iliyopigwa marufuku na NTSA

Mpaka kifo chake, Mohamed Shahid Pervez Butt alitajwa kuwa na utajiri wa Ksh 5Bn, akiwa anamiliki mabasi zaidi ya 209.

Muhtasari

• Kufuatia msururu wa ajali za barabarani, Mabasi ya Modern Coast yalinyang'awa leseni ya kuhusumu na mamlaka ya NYSA.

Mabasi ya Modern Coast
Mabasi ya Modern Coast
Image: Hisani

Mwishoni mwa mwaka jana, waziri wa uchukuzi wa umma na miundo mbinu, Kipchumba Murkomen alitoa agizo kwa mamlaka ya kusimamia usalama wa barabarani NTSA kufutilia mbali leseni za mabasi ya Modern Coast katika barabara za Kenya kufuatia msururu wa ajali zinazohusisha mabasi ya kampuni hiyo.

Lakini je, ni kipi unachokifahamu kuhusu kampuni hiyo ya Modern Coast?

Katika Makala haya, tunakuandalia historia fupi na kampuni ya Modern Coast ambayo kwa mwaka wa 2022 haijakuwa na bahati kufuatia msururu wa ajali za barabarani ambazo zimegharimu maisha ya makumi ya watu.

Makabrasha ya historia yanasema kuwa mmiliki wa kampuni hiyo ni raia mwenye asili ya Kihindi Shahid Pervez Butt, ambaye kwa sasa ni marehemu lakini alikuwa ni Mkenya tajiri wa kunukia pesa, mtu ambaye licha ya utajiri wake, hakuwa anajulikana sana kwani alipenda maisha ya faragha sana.

Kuelekea kifo chake tarehe 11 Julai 2014, alikamatwa kwa madai ya kufadhili shughuli za ugaidi nchini kipindi hicho tishio la Al Shabaab lilikuwa limetanda sana, na aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 akisubiri uchunguzi.

Kulingana na Daily Nation, utajiri wa Shahid ulifikia takriban Shilingi bilioni 5 pesa za Kenya. Alikuwa mmiliki wa kampuni ya Modern Coast Bus Limited, mojawapo ya kampuni zilizofanikiwa zaidi za mabasi yanayosafirisha abiria kati ya Kenya na maeneo mengine ya Afrika Mashariki. Bilionea huyo anasemekana kuwa na magari 209.

Alimiliki Vantage Point Clearing and Forwarding na Vantage Point Transporters. Kampuni hizi za usafirishaji pia zilisaidia wateja kwa usafirishaji wa bidhaa hadi na kutoka bandari ya Mombasa.

Alimiliki nyumba, viwanja na mali za kibiashara katika ukanda wa pwani kupitia kampuni zake-Bluebell properties na Premac Properties. Aliweka pesa zake kwenye akaunti za nje ya pwani. Kando na akaunti katika Kisiwa cha Bermuda, pia alikuwa na akaunti nyingine za akiba na uwekezaji ikiwa ni pamoja na American Express Asset Management.

Mohamed Shahid Pervez Butt aliuawa kwa kupigwa risasi Ijumaa, Julai 11, 2014-mita 300 tu kutoka Kituo cha Polisi cha Changamwe. Tajiri huyo marehemu alikuwa akiendesha gari kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi ambako alikuwa ameenda kumchukua mwanawe Haroun Butt ambaye alikuwa amewasili kutoka London.